Na Lydia Churi, MAELEZO-Dodoma
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka
amewasilisha bajeti ya Wizara yake katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma kwa
kuzitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Wizara hiyo kuwa ni pamoja
na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na nyumba katika maeneo ya mijini na
vijijini.
Profesa
Tibaijuka amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa ardhi
iliyopangwa na kupimwa kwa ajili ya matumizi ya mbalimbali mijini na
vijijini ikilinganishwa na mahitaji pamoja na kuwepo kwa
utamaduni ambao bado hauzingatii mfumo wa ubananaji wa makazi ya mijini
na kasi yake vinavyolazimisha kuheshimu sheria na taratibu za mipango
miji.
Aidha,
Waziri wa Ardhi alisema kubadilisha utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya
ardhi kutoka mfumo usio unganishi kwenda kwenye mfumo unganishi wa
ki-elektroniki ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili wizara yake.
Alisema
changamoto hizi zinakwamisha uendelezaji wa dhana halisi za upangaji,
upimaji na utawala wa ardhi na kuongeza kuwa ili kukabiliana na
changamoto hizo, serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kujenga mfumo
unganishi wa ki-elektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi
utakaowezesha upatikanaji na utumiaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi
kwa ufanisi.
Serikali
pia itaandaa mipango ya matumizi ya ardhi nchini hasa katika vijiji
vilivyopo mipakani na kuendelea kutekeleza programu ya Taifa ya
kurasimisha na kuzuia makazi holela mijini kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali.
Alisema
ili kukabiliana na matatizo ya ardhi, wizara yake itaendelea kuimarisha
vyombo vya kusimamia maadili na weledi wa wataalam wa sekta ya ardhi
katika ngazi zote na kuandaa utaratibu utakaowezesha mamlaka za upangaji kuweka mfumo wa udhibiti na uendelezaji wa ardhi katika ngazi ya kata.
Aidha
Waziri huyo alisema wizara yake itabuni mbinu mpya za kisasa ili kupata
fedha za kuendeleza shughuli za wizara nje ya bajeti kuu ya serikali na
serikali za Mitaa hasa kupitia mikopo ya benki au hisa za makazi.
Profesa Tibaijuka ameliomba Bunge kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya shilingi 101,731,722,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 10,422,891,000 ni kwa ajili ya mishahara , shilingi 71,000,000,000 ni miradi ya maendeleo na shilingi 20,308,831,000 ni kwa ajili ya matumizi mengine.
No comments:
Post a Comment