TFF YAOMBOLEZA MSIBA WA MELI Z’BAR
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea jana (Julai 18 mwaka huu) na
kupoteza maisha ya karibu abiria 100 waliokuwemo kwenye chombo hicho.
Ajali
hiyo mbaya iliyotokea karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar na
kusababisha vifo vya watu wengi ni msiba mkubwa, si kwa wadau wa mpira
wa miguu pekee, bali kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Hivyo
tunatoa pole na salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wote walioathirika na kuguswa na msiba
huo mkubwa.
Kutokana
na msiba huo, mechi mbili za leo kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki
na Kati (Kombe la Kagame) kati ya Atletico ya Burundi na El Salam Wau ya
Sudan Kusini na ile ya Mafunzo ya Zanzibar dhidi ya Tusker ya Kenya
zitachezwa huku wachezaji wa timu zote wakivaa vitambaa vyeusi.
Mbali
ya vitambaa hivyo, pia kutakuwa na dakika moja ya kukaa kimya kwa ajili
ya kuomboleza vifo hivyo kabla ya kuanza mechi hizo zitakazochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi ya kwanza itaanza saa 8.00 mchana
wakati ya pili itachezwa kuanzia saa 10.00 jioni.
No comments:
Post a Comment