Maoni Ya Mnyika (Mb) Kuhusu Hatua Ya Spika Wa Bunge Kuvunja Kamati Ya Nishati Na Madini...!
Kufuatia
uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali
kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa
kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:
Kwa
maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi
kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia
uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa
hautaambana na hatua nyingine za ziada na za
haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa
nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa
serikali.
Ukiondoa
tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya
kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye
kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi
mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge
Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
Hivyo
hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye
wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe
wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya
kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa
dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge
lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo
huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria
wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo
zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya
uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.
Hata
baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye
uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali
kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya
nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio
yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama
nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15
Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.
Nilisema
bungeni kwamba “Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina
ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC
yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge
juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011
yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu
wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya
kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa uzito
unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara
hii hii mara kwa mara”.
Mathalani,
Waziri wa Nishati na Madini ameeleza bungeni tarehe 28 Julai 2012
kuwa wapo wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye kulihujumu
Shirika la Umeme (TANESCO) na Spika wa Bunge akahitimisha kuwa Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itachunguza tuhuma husika na pia
kwamba inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za Maadili (Code of Conduct)
ili kudhibiti hali hiyo.
Hata
hivyo, Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka
2008 baada ya Kashfa ya Richmond iliazimiwa katika Azimio Na. 11,
kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995 (The
Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho makubwa
ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi
Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi
wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali
ianze rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani
na nje ya Bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”
Bunge
lilitaarifiwa Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba
kikundi kazi (Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye
mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura
398) ambao ulikuwa katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu
Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa serikali ilitarajia
kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la
tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama ilivyoshauriwa
na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu azimio hilo
halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.
Aidha,
kumetolewa madai ya baadhi ya wabunge kupokea ama kudai rushwa suala
ambalo nalo Spika wa Bunge ametoa uamuzi kuwa litashughulikiwa na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Lakini Serikali na
Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si mara ya kwanza kwa
tuhuma za namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa kamati
mbalimbali za bunge.
Hata
hivyo, kwa sababu ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa ukamilifu
tuhuma kama hizo zitaendelea kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa kamati
ya bunge ya nishati na madini. Izingatiwe kwamba madai ya rushwa
kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza kuhusu Kamati ya Nishati na
Madini na binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena kwa Kamati Teule
ya Bunge iliyochunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na
Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni mwaka
2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi wabunge kwa rushwa hata hivyo
hatua hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa au kuwachukulia
hatua wahusika.
Suala
hili likatajwa tena na Mbunge wa Kigoma Kaskazini David Kafulila
kuhusu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na likatajwa tena na
Kiongozi wa Upinzani Freeman Mbowe na Mbunge wa Kyela Dr Harrison
Mwakyembe kuhusu uchaguzi wa Afrika Mashariki lakini hatua
hazikuchukuliwa kuchunguza wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo
maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini
kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011
(Maarufu kama Sakata la Jairo), yangetekelezwa na wahusika
wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu pia kwa watendaji wa wizara na
mashirika ya umma kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma
yenye kulenga kuwaathiri wabunge kwa rushwa na maslahi mengine ya
kifedha.
Katika
hali inayoonyeha kwamba Serikali bado haioni uharaka na ulazima wa
kuchukua hatua, wakati bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012
kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi
kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio
hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa
bungeni toka yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011; lakini Waziri akajibu
tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini, bila kujali
kwamba nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali maazimio ya
bunge baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
na ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji wahusika na
kupata pia vielelezo.
Kwa
hiyo, ni muhimu Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea kwenye Hotuba
niliyowasilisha bungeni na kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais, Waziri
Mkuu na Spika wa Bunge juu ya masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na
kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa wabunge kuhusu suala la
ununuzi wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO nilieleza pia
masuala mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu
mabilioni ya shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta
na gesi asili pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa
kuchukuliwa.
Nimetoa maoni hayaleo jumapili tarehe 29 Julai 2012:
No comments:
Post a Comment