AZMA YA KILIMOKWANZA YAONGEZA KASI YA MABADILIKO YA SEKTA KILIMO NCHINI
Na Lydia Churi, MAELEZO-Dodoma
Serikali
imesema mafanikio yaliyotokana na azma ya kilimo kwanza yamesaidia
kuongeza kasi ya mabadiliko ya ukuaji katika sekta ya kilimo nchini.
Akijibu
swali Bungeni mjini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika Adam Malima alisema mafanikio ya kilimo kwanza ni pamoja na
kuongezeka kwa eneo linalolimwa kutoka hekta 264,388 mwaka 2006/2007
hadi kufikia hekta 345,690 mwaka 2010/2011.
Alisema
kuongezeka kwa matumizi ya pembejeo za kilimo kutokana na mpango wa
ruzuku, mbolea kutoka tani 73,000 mwaka 2007/2008 hadi tani 200,000
mwaka 2011/2012, pamoja na mbegu bora kutoka tani 11,056 mwaka 2007/2008 hadi tani 28,612 mwaka 2011/2012.
Aidha, aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa maafisa ugani kutoka
3,000 mwaka 2006/2007 hadi kufikia 7,974 mwaka 2012, ujenzi wa vituo
131 vya rasilimali vya kata pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya zana
bora za kilimo hadi kufikia matreka makubwa 8,466 na madogo 4,571 mwaka
2011.
Naibu
Waziri huyo alisema licha ya kuwepo kwa mafanikio hayo, Kilimo kwanza
kinakabiliwa na changamoto kama vile tija ndogo, ukosefu wa masoko ya
uhakika, ukame na mabadiliko ya tabianchi, miundombinu duni ya barabara,
reli na upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika vijijini.
Alizitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi iliyopimwa
na kuwekewa miundombinu muhimu kama vile maji, umeme na barabara.
Alisema
serikali itashughulikia changamoto hizo kupitia utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo wa miaka mitano na Mpango wa Uwekezaji katika Usalama wa
Chakula Tanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na uwajibikaji kwa maafisa ugani.
Akijibu
swali lililoulizwa na Suzan Lyimo (Viti Maalum) aliyetaka kujua mkakati
wa serikali wa kuwasaidia vijana kujishughulisha na kilimo badala ya
kukimbilia mijini, Naibu waziri huyo alisema serikali inaitazama sekta
ya kilimo kwa mapana yake hivyo inawahamasisha vijana kuanzisha vikundi
vya uzalishaji ili wapatiwe mikopo kwa ajili ya kununua zana bora za
kilimo na kujihusisha zaidi na kilimo ili kuongeza vipato vyao.
No comments:
Post a Comment