ALIYEKUWA
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick
Mwakalebela anatakiwa ajisalimishe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) badala ya kusubiri kukamatwa baada ya vipengele
alivyotumia kukata rufaa dhidi ya kesi yake ya rushwa wakati wa
uchaguzi kutupiliwa mbali baada ya kuonekana havina nguvu mbele ya
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Agosti
mwaka 2010, Takukuru ilimfikisha mahakamani Mwakalebela kwa tuhuma za
kujihusisha na utoaji wa rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni za
ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Iringa Mjini.
Katika
kura hizo, Mwakalebela alimshinda kwa mbali aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
la Iringa Mjini Monica Mbega, hata hivyo alienguliwa kuwania ubunge
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo baada ya Takukuru kumfikisha
mahakamani kwa tuhuma hizo.
Katika
kesi hiyo, Mwakalebela na mkewe Selina, kwa pamoja walikuwa
wakituhumiwa kutoa hongo ya shilingi 100,000 kinyume cha sheria namba
15 (1) , (b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu cha 21 (1) , ( a) na 24 (8) ya
Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.
Mwezi
Mei mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, ilitupilia
mbali kesi hiyo baada ya kusikiliza mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa na
Wakili wa mshitakiwa, Basil Mkwata na kuamuru upande wa jamuhuri
kuifanyia mabadiliko hati hiyo kama wanataka kumfikisha tena mtuhumiwa
huyo mahakamani.
Takukuru
ikiwa katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko hati ya mashitaka,
wakili wa mshatkiwa alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akiomba
mahakama hiyo itolee uamuzi mapingamizi mengine ya kisheria ambayo
Mahakama ya Hakimu Mkazi haikuyatolea uamuzi na mengine ikiyatolea
uamuzi kimakosa.
Hoja
ya kwanza ya wakili wa mshitakiwa iliyosikilizwa na Jaji aliyeendesha
kesi hiyo jana, Rehema Mkuye ilidai, hati ya mashitaka iliyokuwa
imaendaliwa na Jamuhuri haitengenezi kosa la jinai kisheria kwa kuwa
makosa yote kama yalivyokuwa yametajwa kwenye hati hiyo yalikuwa
yanakosa maneno.
Katika
hoja hiyo, Jaji Mkuye alisema mahakama imepitia hoja za pande zote
mbili na kuona hoja hiyo ingekuwa na nguvu kisheria kama mashahidi
wangeitwa na kisha kutoa ushahidi wao.
“Kwa kuwa hilo bado halijafanyika Mahakama Kuu inatupilia mbali kigezo hicho cha rufaa,” alisema Jaji huyo.
Hoja
ya pili ya rufaa hiyo ilieleza kwamba Kifungu cha 21 (1) (a) na
Kifungu cha 24 (8) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi Sheria No 6 ya
mwaka 2010 ambacho mshitakiwa alikuwa ameshitakiwa nacho,
hakikutengeneza kosa la jinai kisheria.
Baada
ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama iliona hoja zote zina
nguvu kisheria lakini Jaji Mkuye alisema kulingana na kifungu cha 359
(2) cha sheria hiyo hiyo, hoja hiyo haikuwa imetolewa uamuzi wowote na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa hivyo haikutakiwa kukatiwa rufaa
kwasababu hakukuwa na amri yoyote ya mahakama ya awali.
“Hivyo
kwa kuwa rufaa iliyokuwa imekatwa na Wakili wa Mwakalebela ilikuwa na
hoja mbili ambazo zote mahakama imezitupilia mbali, hivyo mahakama
inatupilia mbali rufaa yote na amri ya mahakama ya Hakimu Mkazi ya
kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka na kumfikishe tena mtuhumiwa
Mahakamani sasa itatekelezwa,” alisema jaji Mkuye.
Kaimu
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa Stephen Mafipa alisema baadaye
kwamba kikosi chake hakihitaji kumtafuta mtuhumiwa, bali atumie busara
kujisalimisha ili afikishwe mahakamani.
Wakili
wa mtuhumiwa alipofuatwa na vyombo vya habari ili atoe msimamo kwa
niaba ya mteja wake ikiwa ni pamoja na kama watakata rufaa katika
Mahakama Kuu ya Rufani kupinga maamuzi ya Mahakama kuu, hakupatikana
ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment