Watoto zaidi ya 1000 wanufaika na ufadhili wa WAMA
Na Mwandishi Maalum, Abuja
Zaidi ya watoto wa kike na wa kiume elfu
moja ambao ni yatima na wanaoishi katika
mazingira hatarishi kutoka mikoa yote nchini wamenufaika na ufadhili wa masomo unaotolewa na Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo wakati akiongea kwenye mkutano
wa saba wa wake wa marais wa Afrika uliozungumzia masuala ya amani barani
Afrika uliomalizika leo mjini Abuja nchini Nigeria.
Mama Kikwete alisema kuwa kati ya
wanafunzi waliopata ufadhili huo 532 wanasoma elimu ya Sekondari katika shule mbalimbali
hapa nchini, 250 wanasoma shule ya Sekondari ya mfano ya wasichana inayomilikiwa
na Taasisi hiyo ya WAMA-NAKAYAMA iliyopo Rufiji Mkoani Pwani na wanafunzi 12
wanasoma vyuo vya elimu ya juu.
“Taasisi yangu imejenga Shule ya Sekondari
ya kata inayomilikiwa na Serikali ya Nyamisati pamoja na nyumba za walimu ambapo
jumla ya wanafunzi 320 wanasoma katika shule hiyo, pia tumeweza kujenga mabweni
ya wasichana katika shule mbalimbali za sekondari.
Tumechangia elimu kwa kutoa vitabu milioni
moja, madawati, vitanda, magodoro na
kufunga umeme wa jua kwenye baadhi ya shule zisizokuwa na umeme”, alisema
Mwenyekiti huyo wa WAMA”, alisema Mwenyekiti huyo wa WAMA.
Kwa
upande wa afya, Mama Kikwete alisema kuwa
kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) wamekuwa
wakitumia kampeni ya mtoto wa mwenzio ni
wako mkinge na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, ambayo lengo lake kuu ni
kupunguza maambuikizi ya ugonjwa huo kwa watoto na vijana.
Pia
Taasisi hiyo imetoa vifaa mbalimbali vya afya ili kupunguza vifo vya kina mama
wajawazito na watoto katika Zahanati,
Vituo vya Afya na Hospitali 71, kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa mpango
wa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT)
katika mikoa ya Tabora, Pwani, Kagera, Kigoma na
Mtwara.
Mama Kikwete alisema, “Tumeweza kuwasaidia na kuwainua wanawake
kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kutoa msaada wa kifedha kwa vikundi 89 vya Benki za maendeleo
vijijini (VICOBA) na Vikundi vya kuweka Akiba na Kukopa (SACCOs), kutoa mafunzo
ya ukulima wa zao la pilipili aina ya
Paprika kwa wakulima 134 na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake 400
katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Alimalizia kwa kusema kuwa, Taasisi ya WAMA imeweza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa maafisa maendeleo ya jamii katika mikoa ya
Lindi ambao waliweza kuvifundisha vikundi vya wanawake katika maeneo ya vijijini,
kutoa mafunzo ya Ukimwi na virutubisho vya mwili kwa wanawake 100 na usindikaji wa vyakula kwa wanawake 120 katika
mikoa ya Arusha na Pwani.
Taasisi ya WAMA ilianzishwa mwaka 2006
huku ikiwa na malengo ya kumuinua mwanamke kiuchumi, kuhakikisha kuwa watoto wa
kike wanaotoka katika mazingira hatarishi wanapata elimu na kuimarisha afya ya
mama wajawazito na watoto.
No comments:
Post a Comment