JOSEPH SELASINI AREJEA BUNGENI KWA KISHINDO !
MBUNGE
wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), jana alirejea kwa kishindo
bungeni na kupokewa kwa vifijo na wabunge wenzake, baada kupata nafuu
kutokana na ajali mbaya ya gari aliyoipata hivi karibuni.
Nderemo
hizo na vifijo vilianza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu
kumalizika jana asubuhi na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuriarifu Bunge
kuwa mwenzao huyo amerejea.
“Waheshimiwa
wabunge natambua kurejea kwa mwenzetu, Joseph Selasini, ambaye alikuwa
amelazwa baada ya kupata ajali mbaya iliyomsababishia majeraha makubwa
yeye na mkewe na ndugu zake wengine, lakini vile vile katika ajali
hiyo alimpoteza mama yake mzazi, mama mkwe wake, shangazi na dada yake, kweli hilo ni pigo kubwa,” alisema Makinda.
Hata
hivyo pamoja na Makinda kuonesha masikitiko makubwa kwa tukio hilo
baya, wabunge wa pande zote mbili walionekana kumshangilia Selasini kwa
nguvu wakipiga makofi kwa kugonga meza zao.
Makinda alimkaribisha mbunge huyo akisema kuwa wamefurahi kumuona kwani hiyo ni neema ya Mungu kufuatia ajali aliyoipata.
Spika
alimpatia nafasi ya kutoa neno la shukrani na kisha kumfanya
mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya bajeti yaWizara ya Mambo ya Ndani
ya Nnchi, iliyokuwa ikiendelea kujadiliwa.
Selasini
alitumia nafasi hiyo kuwashukuru watu wote waliomsaidia kwa namna moja
au nyingine wakati wote akiwa kitandani na kwenye mazishi ya ndugu
zake, akianza na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
mawaziri, viongozi wa chama chake na vyama vingine, wabunge na
Watanzania kwa ujumla.
“Nawashukuru
wote kwa ushirikiano wenu, upendo wenu mliouonyesha katika familia
yangu wakati nilipopata matatizo na nikiwa hospitalini kwa kweli
nimeuona upendo wenu na sina cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu pekee ndiye
atakayewalipa, asanteni sana,” alisema Selasini.
Akizungumzia
hali ya afya yake pamoja na ya mke wake alisema kuwa anawahakikishia
wabunge pamoja na Watanzania wote na hasa wananchi wa Rombo kwamba afya
zao zimetengamaa kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza
kuwa pamoja na kutengamaa kwa afya zao lakini kuna kitu kimoja tu
ambacho bado kinamsumbua katika mkono wake wa kushoto ambapo bado
amefungwa vyuma.
“Afya
yangu na ya mke wangu imetengamaa kwa kiasi kikubwa na kama alivyosema
mbunge mwenzangu Joshua Nassari kuwa ubunge si kubeba zege, hivyo kama
mnavyoniona pamoja na tatizo la mkono ila mdomo wangu unaongea vizuri
na ninawambia wananchi wa Rombo wasiwe na wasiwasi kwani naendelea
kuwawakilisha vema,” alisema Selasini.
Akichangia
mjadala wa bajeti hiyo, alisema Jeshi la Polisi bado linakabiliwa na
tatizo kubwa la kasma ya kutokuwa na mafuta kwa ajili ya magari, hali
ambayo ni ya hatari sana, ikizingatiwa ukubwa wa kazi yao ya kuzunguka
na kubeba wahalifu.
No comments:
Post a Comment