Monday, July 30, 2012

Mahojiano na Mr. Japhet Kalindu (Afisa Tawala wa Hospitali Ya Igogwe wilayani Rungwe katika mwaka ambao hospitali hiyo inaadhimisha Jubilei ya Almasi (Diamaond Jubilee, miaka 50 ya kuasisiwa).

1.   Tafadhali jitambulishe kwa wasomaji wa Globu ya Jamii kwa kifupi.
Naitwa Mr. Japhet Mwabuluki Kalindu (MPA – HSM, ADHA, Cert. Philosophy) na nimekuwa Afisa Tawala wa Hospitali ya Igogwe kwa miaka 12 sasa- tangu 2000.  

2.   Tupe historia kwa kifupi ya hospitali ya Igogwe:
Ilianza kama Zahanati mwaka 1957. Mwaka 1958 Askofu Van Ooschot aliongea na Masista Wafransiscan wa Uholanzi na Ujerumani kuja Tanzania kejenga na kuendesha Hospitali. Julai 1960 Masista Watatu ambao ni Sr. Tarcisius, Sr. Bonifacio na Sr. Gemma walifika na kuanza kazi mara moja. Uanzishwaji wa huduma za hospitali ulienda sambamba na ombi la wenyeji wa maeneo ya Igogwe kwa sharti kwamba watatoa eneo kujenga Parokia/Kanisa endapo Jimbo litakuwa tayari kuakujenga hospitali. Ndio maana mwaka huo huo 1957 iliponzishwa parokia na huduma za afya zilianzishwa. Kwa haraka sana huduma za afya zilikuwa na watu wengi walifika Igogwe kwa ajili ya kupata huduma. Mwaka 1962 walianza ujenzi rasmi wa hospitali ambayo ilifunguliwa rasmi mwezi Mei 1963. pamoja na ujezi wa hospitali pia walijenga kwa vipindi tofauti zahanati na Kliniki za Mama na Mtoto katika sehemu mbali mbali za Wilaya ya Rungwe na Mbeya vijijini. Katika Wilaya ya Rungwe zahanati zifuatazo zilijengwa na Hospitali ya Igogwe ambazo baadae zilikabidhiwa na Masista kwa serikali: Ibililo, Kipande, Swaya, Ndaga, na Kyimo. Pia walijenga vituo vya chekechea yaani Lubala kilichopo Kijiji cha Lukata, Kiwira na Kanyegele. Vituo vyote hivi vilijengwa ili kusogeza huduma kwa wananchi hasa magonjwa ya akina wakati wa kujifungua.

3.   Hospitali ina uwezo gani?
a.    Rasilimali watu: Madakari wanne (mmoja anasoma surgery), madaktari wasidizi watatu , Afisa Wauguzi Wasaidizi 11, Wauguzi 22, Wateknolojia wanne (wawili maabara, Mfamasia na mmoja Mionzi), Afisa Tawala, Katibu wa Afya, Wahasibu wawili na statistician mmoja na support staff wengi. Kwa ujumla hospitali imeajiri watumishi 120.
b.   Miundombinu: Zipo wodi tano (Wodi ya wanaume na wodi ya wanawake, wodi ya Watoto, wodi ya akina mama, wodi ya Bima, wodi ya magonjwa ya kuambukizwa na wodi ya wagonjwa private. Hospitali ina jumla ya Vitanda 140 vya kulaza.
c.    Throughput: inatibu wagonjwa kati ya 70 hadi 100 kwa siku. Inalaza wagonjwa 5,600 kwa mwaka. Upasuaji kwa mwaka ni 503 kwa mwaka kati ya hizo 182 ni upasuaji wa akina mama wakati wa kujifungua.
d.   Ina uwezo wa kutoa huduma zifuatazo: Huduma za kinga: Huduma ya Uzazi na afya ya Mtoto, Kuzuia Magonjwa ya Maambukizi kama vile UKIMWI nk; Huduma za Tiba: Wagonjwa wa Nje, wagonjwa wa kulazwa na Kliniki ya Wagonjwa wenye maambukizi ya UKIMWI; Promotion and rehabilitation services: Huduma majumbani kwa magonjwa sugu
e.    Uwezo wa hospitali umekuwa ukikuwa katika miaka hamsini ya kuwepo kwake? Kwa vipi? Kama ilivyolezwa hapo awali hospitali imekuwa ikikua kila wakati. Mwaka 1957 kama zahanati, mwaka 1962 hospitali vitanda 40, mwaka 1968 jengo la Watoto Yatima lilikamilika na kuanza kutumika rasmi, miaka ya 1970 ikaongezeka hadi kuwa vitanda 60 pamoja na nyumba za wafanyakazi zilijengwa, jengo la Kliniki likaongezwa mwaka 1974, mwaka 1985 jengo la Maternity na NURU lilikamilika, mwishoni mwa 1990 jengo la kutengenezea maji dawa (Infusions) lilikamilika, Mwaka 1993 jengo la hospitali lilipanuliwa kwa ajili ya maabara ya zamani (sasa chumba cha ultrasound), Upasuaji na mionzi), mwaka 1997 chumba kiliongezwa kwenye wodi ya Watoto kwa ajili ya kitengo cha mionzi ultrasound ambacho kwa sasa ni chumba cha meno, mwaka 1998 nyumba mbili za wafanyakazi zilijengwa zinazoweza kuwa na watumishi 18, mwaka huo huo wa 1998 nyumba wanamokaa Masista wa Jimbo ilikarabatiwa na walianza kuitumia mwishoni mwa 1998, mwaka 2002 nyumba mbili za madaktari zilikamilika, mwaka 2003 jengo jipya la wodi ya magonjwa ya kuambukizwa lilijengwa na kukarabatiwa mwaka 2008, mwaka huo huo wa 2003 kitengo cha Tiba kwa wagonjwa wa UKIMWI kilikarabatiwa, mwaka 2006 jengo jipya la maabara ya kisasa lilikamilika na kuanza kutumiaka, ukarabati wa mara kwa mara umekuwa ukiendelea mwaka hadi mwaka.

4.   Catchment area: Inatibu wagonjwa kutoka katika Tarafa ya Ukukwe Wilayani Rungwe isipokuwa kata ya Malindo. Lakini mara kwa mara tunapata wagonjwa kutoka kote Mkpani Rungwe.

5.   Dhima ya hospitali: Kuendeleza uponyaji alioufanya Kristu katika kuendeleza na kutoa huduma bora za afya kwa wote zaidi sana wale wanaohitaji zaidi msaada wetu.
Hospitali ya Igogwe imekuwa ikitoa mchango mkubwa sana katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. Inahudumia zaidi ya watu 150,000 wanaotoka katika eneo rasmi lililotengwa na Wilaya kwa ajili ya kuhudumiwa na hospitali ya Igogwe kati ya watu 400,000 ndani ya wilaya ya Rungwe. Ni hospitali mojawapo kati ya hospitali tatu zilizopo Rungwe (Itete na Tukuyu). Hata hivyo hospitali inahudumia watu wengi kutoka maeneo mengine ya Wilaya ya Rungwe. Pia Hospitali inatoa huduma zilizo bora kwa wananchi wote ndani ya Mkoa wa Mbeya. Wagonjwa wanaohudumiwa hapa wanatoka wilaya zote za Mkoa wa Mbeya: Mbeya vijijini, Ileje, Kyela, Mbeya Jiji, Mbarali, Mbozi na Chunya. Akina Mama wengi wajawazito wanapenda kujifungulia hapa hasa kutoka wilaya za Mbeya (JIJI na Vijijini), Ileje, Kyela na wachache kutoka Mbarali. Pia wapo wanaohudumia kutoka mikoa ya jirani Iringa, Njomba na Rukwa, na kutoka nje ya nchi kama Malawi na Zambia. Pengo gani amabalo linajazwa na hospitali hii katika utoaji huduma za afya wilayani Rungwe,
Kituo cha Watoto Yatima kinatoa huduma kwa wakazi wote wa Mkoa wa Mbeya na mikoa ya Jirani. Kimekuwa mfano wa kuigwa kwa huduma bora zinasozaidia sana kuwakuza watoto kiafya na malezi bora. Na juzi tu kituo kilingia mkataba kuwahudumia watoto wadogo ambao wamepatikana na wakimbizi wakati taratibu zingine za sheria zinaendelea.

6.   Hospitali ya Igogwe inamiliki ungo wa mawasiliano kwa ajili ya shughuli za mawasilaino ya aina gani hasa?
Ungo unaturahisishia mawasiliano ya aina nyingi. Mawasiliano ya internet kama vile kutuma na kupokea barua pepe, kusoma makala  za fani aina mbalimbali, pia telemedicine. Tulikuwa tunawasiliana na wenzetu wa KCMC kupitia MEMS lakini kwa sasa yamesimama kidogo kwa sababu yule aliyefundishwa hayupo. Telemedecine ni muhimu sana kwa maendeleo ya hospitali katika kutoa huduma iliyobora kwani daktari wa Igogwe aweza kuwasiliana moja kwa moja na daktari wa mahali pengine. Pia hospitali ina mpango wa kuanzisha mawasiliano ambayo daktari wa hapa aweza kuwasiliana na daktari bingwa wa mahali popote duniani na wakashaurinana namna nzuri ya kumhudumia mgonjwa ikiwa ni upasuaji au namna yoyote ile.

7.   Mkoa wa Mbeya una huduma za ‘physiotherapy’ (mama cheza na baba cheza) kwenye hospitali ya Rufaa tu iliyopo jijini Mbeya. Mpango wa hospitali ni kuanzisha huduma hii muhim ili kuwasaidia wananchi wanaohitaji huduma hii wanaotoka maeneo ya wilaya za Rungwe, Kyela, Mbeya Vijini na Ileje.

8.   Changamoto za Hospitali ya Igogwe?
ü  Upatikanaji wa raslimali za kuendeshea hospitali umekuwa mgumu sana: Raslimali watu wachache. Hasa wataalam wa fani mbalimbali (waganga, wauguzi na wafamasia). Imekuwa vigumu kuwaretain watumishi kwani watumishi tulionao wanalipwa kama wale wa serikalini lakini utakuta hapa wanafanya kazi zaidi hivyo wengi hupenda kwenda kufanya kazi serikalini ili wakapumzike kidogo
ü  Raslimali fedha kwa ajili ya kulipa mshahara, kulipa NSSF, kununua dawa, na kufanya shughuliza maendeleo za hospitali
ü  Miundo mbinu imeanza kuchakaa kwani fedha zimekuwa hapa
ü  Kupata kwa wakati fedha za ruzuku kutoka wizarani. Lakini pia wachache ndio wameingizwa kwenye payroll ya serikali hivyo kuipa mzigo mzito hospitali kulipa huduma
ü  Huduma bure kwa mama na mtoto chini ya mika mitano na hali fedha hazitengwi kutoka serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hii kama ilivyoelekezwa kwenye sera. Sera huduma bure, utekelezaji hauonyeshi wapi fungu la fedha kutekeleza hayo
ü  Upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa

9.   Mipango ya hospitali katila miaka 5, 10 au 50 ijayo?
Hospitali katika miaka mitano ijayo imepanga kufanya yafuatayo:

ü  Kuboresha na kuimarisha raslimali watu – kuwalipa vizuri pale inapowezekana na kuwaendeleza
ü  Kutoa huduma bora za afya kwa watu wote hasa akina mama wajawazito na watoto
ü  Kujenga jengo la mionzi (X _Ray)
ü  Kukarabati theatre
ü  Kununua ambulance kufanikisha huduma za rufaa hasa kwa mama mjamzito
ü  Kujenga jengo la maiti
ü  Kuandika maandiko kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba
ü  Kujenga chuo cha waganga
ü  Kujenga nyumba ya masista
ü  Kujenga nyumba za watumishi
ü  Kukarabati jengo la Watoto Yatima
ü  Kukarabati hospitali (wodi na OPD)
ü  Kukarabati nyumba za watumishi
ü  Kujenga jengo la maiti

10.        Ndoto yako: kama ungetokea muujiza wa pesa na rasilimali takribani 100 milioni   zingepatikana ghafla ungezifanyia nini katika Hospitali ya Igogwe leo?
Mungu bariki kama zingefikia 120 millioni ningenunua mara moja gari la kubebea wagonjwa. Kwa 100,000,000 cha kwanza ni kukarabati hospitali na kituo cha watoto yatima kwani majengo yote ya hospitali yamepakwa kwa rangi ya mafuta ambayo ni hatari kama kukitokea janga la moto. Hivyo kubadilisha rangi na kuweka marumalu kwa ajili ya usafi wa hospitali na kituo cha watoto yatima (Tshs 55,000,000), kujenga jengo la mortuary 35,000,000 na kukarabati baadhi ya nyumba za watumishi (10,000,000)

11.       Mipango ya kusheherkea Jubilei ya miaka 50: Hospitali inapanga kufanya nini, lini, wapi kwa nini?
Katika kuadhimisha miaka 50 ya uwepo wa Hospitali ya Igogwe, Hospitali imepanga kuyatekeleza yafuatayo kwa uwezo wa Mungu na msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wenye nia nzuri na hospitali:
ü  Kukarabati Hospitali wodi na OPD Tshs 30,000,000/=
ü  Kukarabati Jengo la Watoto Yatima Tshs 25,000,000/=
ü  Kujenga Jengo la Idara ya Mionzi Tshs 72,000,000/=
ü  Kukarabati Chumba cha Upasuaji Tshs 26,500,000/=
ü  Kujenga jengo la maiti (mortuary) Tshs 35,000,000/=
ü  Kukarabati nyumba za watumishi Tshs 41,400,000/=
ü  Kununua gari la kubebea wagonjwa Tshs 120,000,000/=
ü  Adhimisho la Jubilei Tshs 22,550,000/=

12.        Unauaonaje mgogoro na mgomo wa madaktari na wauguzi uliyotokea hivi karibuni nchini?
Hali tukijua madaktari wanaendeleza kazi ya uumbaji na uponyaji aliyoifanya Mungu hapa duniani na pia wanaendeleza uponyaji wa Kristu, kwa namna yoyote ile mgomo wa madaktari haukuwa mzuri kwa pande zote mbili serikali na madaktari wenyewe kwani watu wengi wameathirika na mgomo huo, kupata ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha. Yafaa pande mbili zikae na kukubaliana ili kulinusuru Taifa. Wagonjwa wengi waliokuwa wamelazwa hospitali kama Mbeya Rufaa walikuja kupata huduma hapa. Japokuwa pato la hospitali huongezeka kwa kuwahudumia wagonjwa lakini pia mzigo uliongezeka sana kwani madaktari na wauguzi waliweza kufanya kazi masaa hata ya ziada ili kuhakikisha wagonjwa wote waliofika wanahudumiwa.

13.       Unatoa wito gani katika kusheherekea Jubilei hii: kwa nani, wito gani, wa aina gani, lini, kwa nini, kwa namna gani?
Naomba Mungu atujalie sote salama katika maisha yetu. Sote tuwe na afya nzuri ili tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri. Naomba Mungu mipango yote iliyo mbele yetu iweze kufanikiwa tena sana na ikiwezekana tupate zaidi ya pale tulipotegemea kwani Hospitali ina mipango mingi lakini kwa ufinyu wa bajeti tunashindwa. Wito wangu kwa wadau wote wote tunashirikiana ili kufanikisha tukio hili kwa ustawi wa watu wetu na taifa kwa ujumla. Kila mmoja achukulie umuhimu wa pekee katika kufanikisha adhimisho hili la Jubilei. Na wale watakaotuunga mkono nawahakikishia kile watakachochangia kitafanya tu yale yaliyopangwa na Kamati na kupata baraka za Baba Askofu Chengula na si vinginevyo. Kushuhudia hili shughuli zote zitakazofanyika zitakuwa wazi kwa wadau wote ili wote waliochangia wajinue kuwa fedha zao ziliingia katika mikono mizuri na kutumika kama ilivyokusudiwa.
Akaunti ya Hospitali kwa ajili ya kuchangia walio mbali na wenye mapenzi mema:

IGOGWE HOSPITAL – JUBILEE AT NBC TUKUYU BRANCH A/C = 038201127120

IGOGWE HOSPITAL – AT NMB TUKUYU BRANCH 1/C = 61403500064

No comments:

Post a Comment