Thursday, July 19, 2012

ICTR YAKATAA MAOMBI YA JOPO LA KUSIKILIZA KILIO CHA WALIOACHIWA HURU

 
Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne alikataa maombi ya watu wanne walioachiwa huru kutaka aunde jopo litakalosikiliza madai yao kuhusu kukosekana kwa nchi za kuwapokea kwenda kuishi.
Rais huyo Jaji, Vagn Joensen amesema amezingatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa ya mahakama hiyo, Novemba 2008 katika kesi ya Waziri wa zamani wa Usafirishaji wa Rwanda, Andre Ntagerura uliotolewa miaka miwili baada ya kuachiwa kwake huru.
‘’Nimelazimika kufuata tafsiri ya sheria kama ilivyotolewa na Mahakama ya Rufaa,’’ alisema Rais huyo wa ICTR.’’ Sheria husika haitoi mamlaka yoyote kwa Mahakama kuyakubali maombi ya walalamikaji. Hivyo sina sababu ya kuunda jopo la kusikiliza maombi hayo,’’ alisema.
Waliowasilisha maombi hayo ni pamoja na mawaziri watatu wa zamani wa Rwanda, Andre Ntagerura(Usafirishaji), Jerome Bicamumpaka (Mambo ya Nje) na Casimir Bizimungu (Afya) pamoja na Brigadia Jenerali Gratien Kabiligi. Wote wanaendelea kuishi mjini, Arusha, Tanzania,makao makuu ya ICTR katika nyumba maalum chini ya uangalizi wa mahakama hiyo.
Katika maombi yaliyotiwa saini na Wakili Philippe Larochelle kutoka Canada, walalamikaji hao wanataka majaji watoe maombi kwa nchi mbalimbali kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wanapatiwa nchi za kuwapokea kwenda kuishi kama watu wengine.
Kwa mujibu wa maombi hayo, Ntagerula anataka kwenda kuishi Canada, Ufaranza au Uholanzi wakati Kabiligi anapenda kwenda Ufaransa. Kwa upande wao Bizimungu na Bicamumpaka wanataka kwenda nchini Canada.

No comments:

Post a Comment