Maganzo: Mji wenye utajiri wa almasi unaotegemea maji ya madumu
Na Joachim Mushi,
Kishapu
KWA mtazamo wa
kawaida ni kitendo cha kawaida kwa mji wowote kuendelea kutokana na rasilimali
zake zinaouzunguka mji huo. Maeneo mengi nje ya nchi na hata Tanzania yamekuwa
yakipata maendeleo ya jamii na mazingira yake kutokana na rasilimali na
shughuli za kijamii zinazolizunguka eneo lenyewe.
Hali hii ni
tofauti na ilivyo katika Mji mdogo wa Maganzo uliopo wilayani Kishapu, Mkoa wa
Shinyanga, ambao umefanikiwa kuwa na rasilimali ghali yenye thamani kubwa
ulimwenguni. Mji huu una madini ya almasi yanayopatikana karibia sehemu kubwa
ya eneo la Maganzo.
Kihistoria Mji wa
Maganzo unachimbwa madini ya almasi tangu kitambo kidogo. Wananchi wanachimba
madini hayo katika mashamba, viwanja na maeneo mengine ambayo yanaaminika kuwa
na almasi. Huu ni utajiri mkubwa ambao Mji mdogo wa Maganzo umefanikiwa kuwa
nao.
Baadhi ya
wananchi wamefanikiwa kunufaika na utajiri huu. Nasema hivyo maana ukifika
katika eneo hilo utashuhudia nyumba za thamani na za kisasa na hata magari ya
kifahari ambayo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameyapata kutokana na almasi.
Mji huo unahuduma
ya umeme, afya (japokuwa kunachangamoto kadhaa), mawasiliano (mtandao wa simu)
na pia umefanikiwa kupitiwa na barabara kuu ya lami inayotoka Shinyanga mjini
kuelekea Mkoa wa Mwanza. Kwa kiasi fulani mji unavutia.
Wapo wawekezaji
kadhaa wa madini akiwemo Kampuni ya Williamson Diamonds ambayo licha ya kumiliki
eneo kubwa la machimbo ya almasi inamiliki maeneo mengine kadhaa ya ndani ya
mji huo. Wachimbaji hawa wanaendesha shughuli za uchimbaji madini eneo hilo.
Lakini pamoja na
rasilimali hii ya Mji Mdogo wa Maganzo hauna huduma ya maji safi na salama ya uhakika.
Mji mzima hauna maji ya bomba na badala yake hutegemea maji ya kuletwa kwa
madumu kwa baiskeli kutoka mjini Mwadui ambapo ni kilometa kadhaa kutoka katika
mji huo.
Wachuuzi wa maji
kwa kutumia baiskeli ndio wanaotoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa
Mji wa Maganzo. Wachuzi hawa zaidi ya 100 ndio wanaotegemewa kuupatia mji huu
maji kibiashara. Dumu moja la maji huuzwa kati ya sh. 400 hadi 500 kulingana na
umbali alipo mwananchi anayeitaji maji hayo.
Benard Lucas ni
mmoja wa wachuuzi (wauzaji wa maji kwa kutumia baiskeli) Maganzo, anasema
alianza kufanya biashara hiyo ya uuzaji wa maji tangu mwaka 2009 baada ya
kupata mtaji. Anasema uuzaji wa maji eneo hilo unaitaji muhusika awe na
baiskeli pamoja na madumu ya kubebea maji pekee.
“Sehemu ambayo
huyachota maji haya sisi hatulipii...huyachota bure kazi yako ni kusafirisha
kwa kutumia baiskeli na kuwatafuta wateja walipo. Dumu moja la maji tunauza
kati ya shilingi 400 na 500 kulingana na umbali anapopatikana mteja,” anasema
Lucas.
Anasema kwa
upande wake huuza madumu 14 hadi 16 kwa siku kulingana na uchakarikaji wa siku
hiyo. Mwanambelembe Machia ni muuzaji mwingine wa maji katika Mji mdogo wa
Maganzo, anasema amekuwa akifanya biashara hiyo kwa muda mrefu sasa na inalipa.
“Mimi nina watu
wangu maalumu ambao tumekubaliana kupeleka maji kiasi fulani kwa kila siku. Huwa
napata wastani wa shilingi 5,000 kwa siku kama kukiwa na biashara mbaya lakini
kiasi hiki kinanitosha kabisa kwa matumizi yangu,” anasema Machia.
Kwa upande wake
Frank Simba mchuuzi wa maji eneo hilo anasema alimaliza elimu ya msingi
mwishoni mwa 2011, lakini baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari
alinunuliwa baiskeli na wazazi wake na kuanza biashara hiyo ya uuzaji maji ili
aweze kujitegemea.
Anasema msimu
mbaya wa biashara hiyo ni kipindi cha masika ambacho wananchi hutegemea maji ya
mvua ili kukwepa gharama. “Kutokana na wingi wetu kipindi hiki huwa kibaya kwa
biashara maana wateja huadimika kabisa,” anasema kijana huyu anaeomba shida ya
maji isitoweke Maganzo.
Hata hivyo Sera
ya Maji ya nchi ya mwaka 2002 inaeleza kuwa madhumuni ya jumla ya sera kuhusu
utoaji wa huduma ya maji vijijini ni kuboresha afya ya jamii na kusaidia
kuondoa umaskini vijijini ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji
safi, salama na ya kutosha.
Madhumuni mahsusi
ya sera hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu ya maji safi, salama
na ya kutosha, kwa gharama iliyo ndani ya uwezo wa wananchi vijijini. Pia
kuweka bayana majukumu na wajibu wa wadau mbalimbali. Lakini kama hiyo haitoshi
sera pia imesisitiza kuhusu wananchi kulipia sehemu ya gharama za ujenzi wa
miradi, na pia kulipia gharama zote za uendeshaji na matengenezo ya miradi yao,
tofauti na dhana iliyokuwepo ya kuchangia tu sehemu ya gharama za uendeshaji na
matengenezo.
Hii haipingwi
kuwa maji ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu. Na kwa kutambua kuwa
upatikanaji wa maji safi na salama ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu,
utoaji wa huduma ya maji vijijini utaimarishwa. Hata hivyo haki kama hii haipo
kwa wakazi wa Mji mdogo wa Maganzo ambao unautajiri mkubwa wa almasi. Wakazi wa
eneo hili kutokana na shida ya maji wamekuwa wakitumia maji kutoka kwenye
madimbwi kukwepa gharama za kununua maji kila kukicha, huku wakihatarisha
maisha yao kiafya.
Mwenyekiti wa Serikali
ya Kijiji cha Maganzo, Lwinzi Kidiga anakiri huduma ya maji ni kero kubwa kwa
wakazi wa vijiji vyote vinavyo zunguka eneo hilo. Anabainisha kuwa zipo juhudi
ambazo yeye na viongozi wenzake wanazifanya kuhakikisha wanakabiliana na hali
hiyo.
Anasema kwa sasa
tayari uongozi wa kijiji umefanya mazungumzo na mwekezaji wa madini ya almasi
eneo hilo, ambaye pia ni mmiliki wa mgodi wa Williamson unaochimba almasi eneo
hilo na mwekezaji huyo amekubalia kuwaletea maji wananchi kwenye moja ya tanki
kubwa ambalo lipo jirani na soko kubwa eneo hilo. Anaongeza kuwa mradi huo
unatarajia kuanza kati ya mwezi Julai, 2012.
Lakini huenda
miaka kadhaa ijayo kero hiyo ya maji ikatoweka kwani, Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Lucas Said akizungumzia kero hiyo anasema kwa
sasa wataalamu wanafanya utafiti katika vijiji kadhaa kuhakikisha vinapatiwa
huduma ya maji pale mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria kwa matumizi
eneo hilo utakapo kamilika.
Makala
haya yameandaliwa na mtandao wa Thehabari.com- www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment