NEWS UPDATES:::WASHTAKIWA WA EPA WAFUNGWA JELA MIAKA 18
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha
miaka 18 jela Kada wa CCM, Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala
Hussein katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh2.2 bilioni za Akaunti ya
Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mahakimu wawili katika jopo la waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo
waliwatia hatiani watuhumiwa kwa makosa sita kati ya saba yaliyokuwa
yakiwakabili na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.
Kwa upande wake kiongozi wa jopo hilo, Jaji Fatuma Masengi aliwaachia
huru washtakiwa hao kwa maelezo kwamba upande wa mashtaka ulishindwa
kuthibitisha mashtaka yote saba yaliyokuwa yanawakabili.
Hata hivyo, hukumu hiyo haikuweza kuwaokoa watuhumiwa na hasa Farijala
na Maranda watatumikia adhabu yao kwa miaka mitatu jela kwa kuwa adhabu
zote walizopewa zitakwenda kwa wakati mmoja.
Tayari Maranda na Farijala wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitano
jela, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za EPA,
ambapo walihukumiwa na mahakama hiyo Mei 23, 2011.
Jopo lagawanyika
Jopo la mahakimu watatu lililokuwa likisoma hukumu hiyo liligawanyika
na kusoma hukumu mbili tofauti, ambapo hukumu moja iliyoandaliwa na
kusomwa na kiongozi wa jopo hilo, Jaji Masengi aliyewaachia huru
washtakiwa.
Hata hivyo, katika hukumu ya pili, iliyoandaliwa na Hakimu Projestus
Kahyoza na mwenzake Catherine Revocate iliwatia hatiani washtakiwa
katika makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili, na kuwahukumu
kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa.
Hata hivyo, wakati wakisoma hukumu hiyo, mahakimu hao walisema badala
ya washtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 18, hukumu yao itaenda
sambamba hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Kabla ya hukumu
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, hakimu Kahyoza na mwenzake walipitia
ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka akiwamo
mtaalamu wa maandishi, Joseph Mgendi ambaye aliweza kuangalia saini
katika nyaraka halisi na zinazodaiwa kughushiwa, ikiwamo hati ya
usajili ambapo alibainisha kuwa zilikuwa zimeghushiwa.
Pia walipitia utetezi uliotolewa wa mshtakiwa Maranda, ambaye aliyakana
mashtaka yote saba yanayowakabili na kwamba, alikataa katakata kuwa
hakuwahi kula njama na kughushi hati ya usajili wa Kampuni ya Money
Planners & Consultant.
Hakimu Kahyoza alisema, Maranda alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda Brela
kusajili kampuni hiyo na kwamba, aliyewahi kwenda kusajili kampuni ni
binamu yake, Farijala.
Hakimu Kahyoza alisema, Maranda katika utetezi wake alisema yeye
hakuwahi kughushi hati yoyote hivyo, haikuwa rahisi kwake kutoa hati
iliyoghushiwa pia, hakuwahi kuiba fedha BoT na wala hakuwahi kujipatia
fedha yoyote kwa njia ya udanganyifu.
Kahyoza alifafanua kwamba, Maranda alidai mfumo uliotumika kuwaingizia
fedha kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CBA uliendeshwa
kihalali ndiyo maana, BoT hawakuwahi kulalamika hivyo, aliiomba
mahakama imuone hana hatia.
Akisoma utetezi uliotelewa na Farijala, Hakimu Kahyoza alisema,
Farijala naye alikataa madai ya kughushi, kuwasilisha nyaraka bandia
benki, kuiba fedha yoyote na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na
aliiomba mahakama imwachie huru kwa sababu hana hatia.
Yasiyo na utata
Hakimu Kahyoza alisema kuwa mahakama ilibaini kuwapo kwa masuala
yasiyokuwa na utata ambayo ni pamoja na kwamba Maranda na Farijala ni
ndugu, waliwahi kufanya biashara pamoja na waliingiziwa fedha kwenye
akaunti namba 0101379004 ya United Bank of Africa ambazo ni kiasi cha
Sh2.2 bilioni.
“Baada ya kuweka msingi huo, mahakama ilijiuliza je, washtakiwa
walikula njama ya kuiibia BoT, walighushi hati ya usajili wa kampuni
namba 150731, walighushi hati ya mkataba kati ya Kampuni ya Money
Planners & Consultant na Kampuni ya B. Grancel ya nchini
Ujerumani, waliwasilisha nyaraka za kughushi benki, waliibia BoT na
kwamba je, walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,” alihoji Kahyoza.
Hakimu huyo alisema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, hakuna utata
kuwa hakuna mahali panapoonyesha washtakiwa ndiyo walikuwa wamiliki wa
kwanza wa kampuni hiyo Money Planners & Consultant na kwamba majina
yanayodaiwa kuwa ni wamiliki wa kampuni hiyo ya Thobias Kitunga na
Paulo ni majina ya uongo na ya kufikirika.
Alisema licha ya majina hayo kuwa ya kufikirika, mabadiliko ya kampuni
hiyo ya Money Planners & Consultant hayakuwahi kufanyika na hata
Brela hakuna kumbukumbu, hivyo saini zilizopo katika nyaraka za kampuni
hiyo ikiwamo hati ya usajili ni za kughushi.
Alisema sababu ya kuthibitisha hilo ni kwamba, ofisi ni ileile iliyopo
Magomeni Mapipa, Mtaa wa Iramba nyumba namba 7 hata baada ya
mabadiliko.
“Hati hizo za usajili hazikusainiwa na Msajili wa Biashara toka Brela,
Noel Shani bali zilisainiwa na washtakiwa wenyewe. Hivyo, kwa mujibu wa
kifungu cha 333 na 335 (c) (e) vimetufanya tufikie hitimisho kuwa
washtakiwa walighushi nyaraka hizo,” alisema Hakimu Kahyoza.
Alisema Maranda na Farijala walighushi hati ya mkataba ya Septemba 8,
2005, wakitumia majina ya Thobiasi na Paul na kwamba hati hiyo
haikusainiwa na Kampuni ya Money Planners & Consultant.
“Maombi ya kupewa fedha hizo Sh 2.2 bilioni, yalipitiwa na watu kadhaa
wakiwamo Mwanasheria wa BoT na kupeleka kibali cha mwisho kwa Gavana
aidhinishe malipo, hakuna hata mmoja aliyebaini kuwa katika hati ya
mkataba kati ya Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani na Kampuni ya
Money Planners & Consultant, haikuwa na saini ya Kampuni ya Money
Planners & Consultant,” alisema.
Aliongeza: “Kwa sababu hiyo inaonyesha wazi, washtakiwa ndiyo
walighushi nyaraka hizo hivyo hati ya usajili wa kampuni hiyo, hati
ya mkataba ni za kughushi.”
“Tuna haki ya kuamini kuwa washtakiwa kwa kujua, walifanya hivyo kwa
nia mbaya ya kuwasilisha hati hizo za kughushi CBA na baadaye BoT”,
alisema Kahyozi.
Alisema hakuna ubishi kuwa hakuwapo hata shahidi mmoja aliyewahi
kuthibitisha kuwa washtakiwa hao waliwahi kuiibia BoT Sh 660,210,000.
“Katika hili hatupo tayari kukubaliana na upande wa mashtaka kwa sababu
halijathibitika”.
Aliongeza kwamba, hakuna utata kuwa BoT iliweka kwenye akaunti ya
washtakiwa zaidi ya Sh2.2 bilioni na kwamba, kiwango hicho cha fedha
kiliwekwa baada ya washtakiwa kuwasilisha hati za kughushi katika benki
hiyo kuu ikiwamo hati ya usajili na hati ya mkataba.
Hakimu alisema kulikuwapo na maofisa wa juu BoT waliotakiwa
walithibitishe hilo, lakini, Mwanasheria wa BoT yeye alikuwa
anathibitisha uhalali wa hati hiyo ya mkataba ambayo haikusainiwa
upande mmoja na Kampuni ya Money Planners kuwa, “Ina nguvu kisheria
hivyo, inaweza kutumiwa na BoT kuhamisha au kuchukua fedha
zinazoongelewa katika maombi ya washtakiwa”.
Alifafanua hakimu, “Mwanasheria alimaanisha kuna watu wengine
walithibitisha, sisi kwa mtazamo wetu ni ajabu kwa maofisa hao hata
mmoja hakuwahi kuona katika hati ya mkataba hakuna saini ya Kampuni ya
Money Planners.
Tunajiuliza walimezwa katika huu mtego au walipumbazwa? Kama
walipumbazwa, upumbazo huo ulikuwa ni wa hali ya juu na kujikuta wote
wanaingia kwenye mtego huu.” alisema Hakimu Kahyoza.
Aliongeza kwamba washtakiwa hao walifanya matendo hayo yote kwa nia
mbaya na kuwafanya watu wengine, wawe sehemu ya kughushi.
Kuhusu shtaka la kula njama, kwa ujumla maelezo yote yanaonyesha
Maranda na Farijala, walikubaliana makazi ya ofisi yawe Magomeni, Mtaa
wa Iramba nyumba namba 7 ambako ni nyumbani kwao, waliwasiliana,
walikutana, walijadiliana hivyo walitenda kosa la kula njama.
“Sisi hatuna sababu za kusitasita kuwa kweli washtakiwa walikula njama
dhidi ya BoT. Ni kweli walikula njama,” alisisitiza Kahyoza.
Jaji Masengi
Kwa upande wake, Jaji Masengi aliwaachia huru washtakiwa wote kwa
sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuyathibitisha mashtaka yote saba
yanayowakabili.
Jaji Masengi alisema BoT ndiyo wangekuwa walalamikaji wakuu, lakini
haikuwahi kulalamika kutoa fedha hizo zinazodaiwa kuibwa na washtakiwa
wala Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani.
Kuhusu kughushi, alisema ushahidi uliotolewa haukutosheleza
kuthibitisha kosa hilo na kwamba licha ya utetezi kuwa na upungufu
lakini hakukuwa na sababu za kuwatia hatiani.
Kabla ya hukumu
Kabla ya kusomwa kwa hukumu ya Hakimu Khayoza na Hakimu Catherine,
Wakili wa Serikali, Alapha Msafiri aliiambia mahakama kuwa washtakiwa
siyo wakosaji wa mara ya kwanza, wanatumikia kifungo cha miaka mitano
jela katika kesi namba 1161 ya mwaka 2008.
Msafiri aliiomba mahakama itumie kifungu cha 348 na 358 cha Makosa ya
Jinai (CPA), kutoa amri Maranda na Farijala walipe fidia au warejeshe
kiasi walichojipatia kwa njia ya udanganyifu.
Wakili Majura Magafu, anayewatetea Maranda na Farijala, alidai kuwa ni
kweli washtakiwa walitiwa hatiani lakini, isiwe kigezo cha kuwapa
adhabu kali kwa sababu kesi namba 1163 na 1161 zilifunguliwa siku
moja, zinahusu makosa ya aina moja isipokuwa zilipangiwa jopo tofauti.
“Hii ni tofauti na mtu aliyetenda kosa akaachiwa halafu akafanya tena
kosa lingine, pia mazingira ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa
yalikuwa na utata kwa namna moja au nyingine na kwamba washtakiwa
walitenda makosa bila ya kujua kama wanatenda makosa,” aliwatetea
wakili huyo na kuongeza:
“Kwa hiyo ni dhahiri, matukio hayo hayakufanyika kwa makusudi kwa
asilimia 100, kwa kuwa wao waliamini ni halali lakini baadaye
ilibainika kuwa si halai”.
“Waheshimiwa washtakiwa wote wana matatizo ya kiafya, Farijala ana
matatizo ya presha ya macho na Maranda ana tatizo la Figo, naomba kama
mahakama itaridhia chini ya kifungu cha 38, ina mamlaka ya kuangalia
mazingira ya utendwaji wa matukio, hali za watuhumiwa na kuwaachia
kwa masharti maalumu kutokana na afya zao,”alisema Magafu.
Pia aliiomba mahakama itamke wazi wazi kuwa adhabu watakayopewa
washtakiwa kama itakuwa ni ya kifungo, inastahili kuanza lini kwa
sababu kumekuwapo na utata wa sheria, kuwa ni lazima wamalize kifungo
cha awali ndiyo waanze kingine.
Kwa upande wa Hakimu Catherine Revocate, alisema wamejadiliana kwa
kuangalia mazingira ya kesi, afya za washtakiwa na kwamba ni wakosaji
wa mara ya kwanza kwa sababu kesi hiyo inasimama peke yake, katika
shtaka la kwanza hadi la saba kasoro shtaka la sita waliloachiwa huru;
washtakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka mitatu katika kila kosa.
No comments:
Post a Comment