Thursday, July 19, 2012

WAZIRI WA MAJI PROF MAGHEMBE AAHIDI KUSHUGHULIKIA UPUNGUFU WA HUDUMA YA MAJI SUMBAWANGA, KALAMBO

Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe(kushoto) akisalimiana na Afisa Maendeleo wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Crispin Luanda kulia


NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI-SUMBAWANGA

SERIKALI imewataka wananchi kuacha utamaduni wa kuchoma misitu moto

ili kuhifadhi mazingira, ikiwa ni pamoja na kuwa na vyanzo endelevu
vya ikiwemo mito ya asili.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maji Mheshimiwa Profesa Jumanne

Maghembe wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ulumi Kata ya
Ulumi wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, wakati wa ziara yake mkoani humo
kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Alisema hayo baada ya kupokea taarifa ya mradi wa maji unaotarajiwa

kutekelezwa na Halmshauri ya wilaya ya Sumbawanga kijijini hapo,
ambapo chanzo cha maji ya mradi huo ni mto Kapoka.

Alisema endapo wakazi wa kijiji hicho hawataacha uharibifu wa misiti

katika maeneo ya mto huo,  huenda ukakauka katika kipindi kifupi
kijacho, hali itakayosababisha tatizo la upungufu wa huduma ya maji
kuendelea katika kijiji hicho.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Maghembe aliwashauri wataalamu wa Maji

wa Halmashuri ya Sumbawanga ambayo inahudumia wilaya mbili za
Sumbawanga Vijijini na Kalambo kufanya utafiti ili kubaini vyanzo
vingine vya maji kijijini hapo kuliko kutegemea mto huo pekee ambao
uhai wake uko mashakani endapo uharibifu wa mazingira hautadhibitiwa
kikamilifu.

Waziri huyo wa Maji aliahidi kupambana na tatizo la upungufu wa maji

linalowakabili wakazi 4791 wa kijiji hicho, ambao kwa sasa wanategemea
chanzo kimoja tu cha maji hali inayopelekea upungufu wa huduma hiyo.

Aliwaahidi wakazi hao kuwa, katika kipindi cha wiki moja ijayo

wataalamu wa maji wataanza kazi ya kutafiti vyanzo vingine vya maji
kijijini hapo, ambapo alisema eneo hilo linaoekana kuwa na maji mengi
ardhini.

Alisema kuwa, kazi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya

Laela, Matai, na Nankanga pia utaanza mara moja, na kwamba nia ya
serikali ni kusambaza maji katika maeneo yote nchini ambayo
yanakabiliwa na upungufu wa huduma hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment