WATANZANIA WATAKIWA KUUDHAMINI UTAMADUNI WAO
Msanii
wa Ras Innocent Nganyagwa akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki
hii. Kushoto kwake ni Afisa Habari Mkuu BASATA Bi Agnes Kimwaga.
Mkurugenzi
wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari kutoka Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) Godfrey Lebejo akisisitiza jambo wakati akihitimisha
programu ya Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Watanzania
wametakiwa kuuenzi utamaduni wa makabila ambao una thamani kubwa sana,
wito huu umetolewa wiki hii kwenye ukumbi wa BASATA na mwanamuziki
mkongwe wa regge nchini na mtafiti mbobevu wa masuala ya historia za
jamii, Innocent Nganyagwa, alipokuwa akiwasilisha mada katika Jukwaa la
Sanaa kuhusu Umuhimu wa Utafiti Wa Makabila Katika Kuendeleza Utamaduni Wetu.
Alisema tamaduni za makabila mengi ya Tanzania zina mashiko mazuri na yenye thamani ambayo yakienziwa na kuendelezwa, yatawasidia watu katika maendeleo ya sasa.
Alisema Watanzania tunapaswa kujitambua na kujua mashiko ya Sanaa na tamaduni zetu na kuhuisha thamani ya maadili yetu kitaifa.
“Kila
kabila lilikuwa na taratibu zake na mifumo yake ya utawala na shughuli
zake za uchumi, pia makabila mbalimbali yalishirikiana, mambo haya
yakiendelezwa ni dhahiri tunaweza kuendela zaidi katika zama za sasa za
changamoto za utandawazi, uliorahisisha maendeleo lakini pia ukatuletea
baadhi ya tamaduni za kigeni zinazopotosha maadili.
Msanii
huyu aliwataka Watanzania kufanya tafiti zaidi na kujitambua wao ni
nani na asili yao ni nini ili wasitegemee historia zilizoandikwa na
wageni peke yake, kwani nyingi zinaishia katika mazungumzo waliyopewa
bila kushiriki kikamilifu katika kupata taarifa zaidi za historia hizo
kwa kuzipima katika ‘mzania jumuishi’ wenye kina kirefu cha mila na
desturi.
Nae
Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, ndugu Lebejo, alisistiza kuwa
tungeendeleza kilichopo kwenye tamaduni zetu na kukichanganya na
teknolojia tungefika mbali sana katika kila eneo, tushikilie mila zetu
tusiige vya Wazungu kwani wao wana mila zao na wanaziendeleza kwa mujibu
wa mashiko yao ya utamaduni wao, tusibweteke na kupenda vya kuiga vya
kigeni wakati tuna mambo yetu mengi yenye thamani na mafundisho ya
kuishi maisha sadifu ya kimaadili.
“Tujitambue
na kuzifahamu mila zetu kwa kufanya tafiti, tusisubiri mpaka tuwe
maprofesa ili kuweza kufahamu tulikotoka, kwani mengi kati ya yanayohusu
utamaduni wetu yanatuzunguka katika maisha yetu ya kila siku. Ni suala
tu la kuwa na mtazamo chanya na kuamua kwa dhati kuuenzi utamaduni
wetu”,alisisitiza ndugu Lebejo.
No comments:
Post a Comment