SMZ KUIMARISHA VYOMBO VYA USAFIRI
Na Khadija Khamis –Maelezo
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuchukua hatua kadhaa za kuimarisha vyombo vya usafiri ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inaimarika kwa kupatiwa vyombo vya kisasa nchini .
Akijibu suala la Mwakilishi, Asha Abdu Haji nafasi za wanawake huko katika ukumbi wa baraza la wawakilishi Mbweni aliyetaka kujua hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kuondoa usumbufu wa usafiri kati ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Waziri
wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad alisema kwa ujumla
suala la usafiri kwa Unguja na Pemba limekuwa ni tatizo la muda mrefu
kutokana na meli kubwa za serikali kuchakaa na kuharibika mara kwa mara
na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi .
Aidha alisema serikali ina nia ya kuruhusu kuwepo kwa biashara huria kwa kuwapa mwamko wafanyabiashara kuanzisha biashara hiyo lakini inaonekana kuwa bado mwamko huo ni mdogo .
Waziri
huyo alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara walionyesha nia ya
kukubaliana na Serikali kwa kuanzisha ruti za Unguja na Pemba ingawa
kumekuwa na matokeo yasiyoridhisha lakini atahakikisha kuwa huduma ya
usafiri inaimarika nchini.
Hamad alieleza kuwa serikali itaendelea kuwashajihisha wafanyabiashara ili kuona umuhimu wa kununua meli mpya na zilizosalama zaidi kama taratibu za usafiri baharini zinavyoelekeza katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza .
‘’Tukipata meli hizi mpya kubwa na za kisasa changamoto zilizopo zitaondoka’’ alisema Hamad .
Alisema kuwa sababu nyingi zinazojitokeza na kuleta usumbufu katika
usafiri wa bahari ikiwemo uchakavu wa meli, ubovu, masuala ya kiufundi
pamoja na hali ya hewa ambavyo huchangia kuwepo kwa matatizo hayo.
Waziri wa Miundombinu alieleza kwamba serikali inachukuwa hatua za kuondoa usumbufu huo kwa kuhakikisha kwamba wahusika wote wanafuata sheria ziliwekwa katika vyombo vya usafiri baharini .
Aidha
serikali imetoa wito kwa wafanyabiashara kuwekeza katika vyombo vya
usafiri hata hivyo inafanya jitihada ya kupata meli nyengine mpya,
ambayo itakuwa kubwa ya kisasa itakayokidhi mahitaji ya huduma za
usafiri kati ya Unguja na Pemba.

No comments:
Post a Comment