Wakati
16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inaanza Jumamosi (Julai 7
mwaka huu) timu 14 zitakazocheza hatua hiyo zimeshajulikana baada ya
mechi zilizochezwa leo (Julai 5 mwaka huu) katika viwanja vinne tofauti.
Tanga
iliyoigaragaza Kaskazini Pemba mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam imechukua moja kati ya
nafasi nne kutoka kundi B. Mabao ya Tanga yalifungwa na Mbwana Musa
dakika ya 30, 55 (penalti) na 58 wakati lingine lilifungwa dakika ya 53
na Issa Mwanga.
Kwa
ushindi huo, Tanga iliyofikisha pointi tisa inaungana na Mjini
Magharibi yenye pointi 13, Morogoro pointi 12 na Mwanza pointi 11 kutoka
kundi hilo kucheza hatua ya 16 bora.
Mara
iliyoichapa Mtwara mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko
Kawe, Dar es Salaam na kufikisha pointi tisa nayo imepata tiketi ya 16
bora kutoka kundi C ikiungana na Dodoma yenye pointi 12, Kinondoni
pointi 11 na Temeke pointi tisa.
Mabao
ya Mara ambayo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa
3-0 yalifungwa na George William dakika ya pili, Edson Mwara dakika ya
17 na 45, na Hassan Ally dakika ya 88. Mtwara walipangusa machozi dakika
ya 36 kwa bao la Ramadhan Njunja.
Ndoto
za Ilala kucheza 16 bora zimeyeyuka baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya
vinara wa kundi A Ruvuma kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mbali ya
Ruvuma iliyofikisha pointi 16, timu nyingine zilizopata tiketi ya 16
bora kutoka kundi hilo ni mabingwa watetezi Kigoma wenye pointi 12,
Rukwa pointi kumi na Arusha pointi nane.
Mchuano
wa kupata timu mbili za mwisho kucheza 16 bora uko katika kundi D
ambalo linasubiri matokeo ya mechi ya leo jioni kati ya Kusini Unguja na
Tabora itakayochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.
Kagera
ambayo leo imeifunga Shinyanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu ni
moja kati ya mbili ambazo zimeingia 16 bora kutoka kundi hilo. Nyingine
ni Kilimanjaro iliyoongoza kwa kufikisha pointi 18 ikifuatiwa na Kagera
yenye pointi tisa.
Nafasi mbili zilizobaki zinawaniwa na Pwani yenye pointi saba, Singida (7), Tabora (6) na Kusini Unguja yenye pointi nne.
No comments:
Post a Comment