Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa mikakati ya
kudhibiti dawa za kulevya ili kuweza kupambana na uingizwaji na utumiaji
wa dawa hizo nchini .
Akijibu suala la Mhe Ismail Jussa ladhu jimbo la mji
mkongwe alietaka kujua hatua gani zinachukuliwa na Serikali kuweza kudhibiti
madawa ya kulevya nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa
Rais ,Fatma Abdulhabib Fereji alisema wizara yake itahakikisha
mikakati hiyo inafanyakazi ili kuona Zanzibar inakuwa salama na utumiaji
wa dawa za kulevya.
Amesema janga la dawa za kulevya halina mipaka na
kuathiri mustakbali wa rasilimali na nguvu kazi ya taifa, hivyo juhudi
zinahitaji kuchukuliwa katika kuzuiya matumizi ili kuwaepusha vijana
kutumbukia katika janga hilo.
Mh. Fatma amesema katika kipindi cha mwaka 2010 kuanzia
novembar hadi disemba ni kesi 67 zilizokamatwa na januari 2011 hadi
juni 2011 ni kesi 168 na kuanzia julai 2011 hadi juni 2012 ni kesi
104.
Alieleza kuwa katika harakati hizi za kupambana na
udhibiti wa dawa za kulevya na uhalifu kwa ujumla umepungua
kutokana na kuimarisha ulinzi shirikishi na taasisi za dola
kufanya doria mitaani pamoja na kuandaliwa kikosi maalum kikosi kazi
ambacho hufichua maficho ya watumiaji na wauzaji dawa za kulevya .
Fereji alivitaka vyombo vya dola vilivyopewa majukumu
ya kupambana na tatizo hilo kuengeza kasi za utendaji kazi zao ili kunusuru
vijana wa taifa letu ambao ni wahanga wakubwa katika janga hili
Waziri huyo alieleza kwamba kwa kutambua mchango wa
taasisi zisizo za kiserikali katika suala zima la mapambano dhidi ya
dawa za kulevya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais (OMKR ) kupitia tume
ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya ilizipatia jumla ya shilling
million tisa na laki tisa (9,900,000/-)nyuma tisa za makaazi ya vijana
wanaoacha matumizi ya dawa ya kulevya (sober house)Unguja na Pemba ambazo
zinatumika katika malipo ya kodi za nyumba chakula na vifaa vyengine
vidogo vidogo vya nyumbani .
Aidha alisema kuwa Ofisi hiyo imeweza kutoa msaada
wa vifaa vya Elektronik ikiwemo Televisheni na Radio kwa Sober house
kwa Unguja na Pemba pia imeweza kutoa mafunzo mbali mbali juu ya uongozi
,utunzaji kumbukumbu na fedha yameweza kutolewa kwa viongozi wa makaazi
hayo kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uwiano mzuri wa kuweza kukabiliana
na vijana ambao wanaoishi huko ili kuweza kutoa huduma zenye kuleta
ufanisi.
Waziri huyo alisema kuwa Wizara yake itaendelea
kuunga mkono juhudi hizo na kutoa wito kwa taasisi nyengine mbali mbali
na jamii kwa ujumla kuendeleza kutoa msukumo wa michango yao ya kuweza
kuendeleza mbele harakati hizo .
No comments:
Post a Comment