Friday, July 13, 2012

KOCHA CAMEROON ATAKA ETO'O AVULIWE BEJI YA UNAHODHA

Mshambuliaji na nahodha wa Cameroon, Samuel Eto'o
  
YAOUNDE, Cameroon

KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Denis Lavagne ametaka mshambuliaji Samuel Eto'o anyang’anywe unahodha wa kikosi hicho pindi atakaporejea kikosini kutoka kufungiwa na Shirikisho la Soka la nchi hiyo (CFF).

Eto'o alifungiwa kutocheza timu ya taifa kwa miezi minane kwa kuongoza mgomo Novemba mwaka jana, wakati Cameroonilipokataa kucheza kirafiki na Algeria kwa sababu ya kushinikiza utekelezaji wa malipo ya posho walizoahidiwa.

Katika barua yake kwa CFF, Lavagne raia wa Ufaransa amelitaka shirikisho hilo kufanya maamuzi juu ya beji ya unahodha wa Eto’o kabla ya mechi za mwisho za hatua ya awali kufuzu Mataifa Afrika 2013 dhidi ya Cape Verde Islands hapo Septemba na Oktoba.

"Kwa hiyo, tunaomba mkutano wa kuthibitisha uteuzi wa nahodha mpya wa timu ya taifa na msaidizi," aliandika Lavagne katika barua aliyoionesha kwa vyombo vya habari vya Cameroon.

Aidha, Lavagne alilalamika kwamba mshahara wake wa dola 245,000 hajalipwa hadi sasa na CFF, na kwamba makubaliano katika mkataba yalitaka alipwe pesa hiyo kwa pamoja. 

Lavagne, aanakumbukwa kwa tamko lake la hivi karibuni alilitoa la kulionya shirikisho la soka la nchi hiyo kwa kukosa heshima kwa waziri wa serikali anayehusika na michezo.

Mfaransa huyo alipewa mikoba ya kuinoa Cameroon mwaka jana, baada ya vigogo hivyo vya soka kumtimua Mhispania Javier Clemente aliyeshindwa kuipeleka nchi hiyo katika fainali zilizopita za Mataifa Afrika 2012 huko Equatorial Guinnea na Gabon.

No comments:

Post a Comment