KESI YA 'LULU' YAAHIRISHWA HADI JULAI 9 2012
UMRI
wa Msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael ‘Lulu’ unaendelea kupigwa
danadana baada ya leo asubuhi upande wa Jamhuri katika kesi hiyo
kukimbilia Mahakama ya Rufani kuomba uhalali wa Jaji wa Mahakama Kuu
kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Kwa
sababu hiyo Jaji Dk. Fauz Twaib alishindwa kuendelea kusikiliza kesi
hiyo ambayo pande zote zilishapeleka ushahidi wake hivyo ilikua kazi ya
jaji huyo kufanya uchunguzi na kutoa uamuzi wake.
Katika
mdai yake kwa Mahakama ya Rufani upande wa Jamhuri umeeleza kwamba
kitendo anachotaka kufanya jaji Dk. Twaib si halali na kwamba kulikua na
upungufu wa kisheria hivyo kuitaka mahakama hiyo kusema iwapo ni halali
ama la.
Akiahirisha
kesi hiyo hadi Julai 9 mwaka huu jaji huyo alizitaka pande zote
zisubiri iwapo faili la kesi hiyo litaitwa Mahakama ya Rufani huku
upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama ukihoji sababu
za Jamhuri kukimbilia Mahakama ya Rufani jana huku ukieleza kwamba
kulikua na muda wa kutosha kufanya hivyo.
Awali
Mwanasheria wa Serikali Elizabeth Kaganda aliomba apewe muda wa dakika
10 ili aangalie iwapo faili la kesi hiyo limeitwa Mahakama ya Rufani
akidai kuwa yapo masuala yanayohitaji mwongozo wa mahakama hiyo.
Nje
ya mahakama hiyo wakili mwingine wa utetezi katika kesi hiyo Peter
Kibatala alidai kwamba wakati kesi ilipokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu waliomba mshitakiwa apewe haki sawa na mtoto ombi lililopingwa na
upande wa Jamhuri kwa maelezo kwamba mahakama hiyo haikuwa na mamlaka
ya kusikiliza ombi hilo.
“Sisi
tumewasilisha uthibitisho kuhusu umri wa Lulu na upande wa Jamhuri nao
tulisikia wamefanya hivyo leo tukaja kwa ajili ya uamuzi lakini imekuwa
ndivyo sivyo,” alilalama wakili Kibatala.
Lulu
anatuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba yaliyotokea
Aprili 7, 2012 huku upande wa utetezi ukidai kwamba msanii huyo ana umri
wa chini ya miaka 18 jambo linaloendelea kuzua ubishani mahakamani.
Katika
kesi hiyo upande wa jamhuri unaongozwa na Kaganda akishirikiana na
Shadrack Kimaro wakati Fungamtama, Kibatala na Fugency Massawe
wakimtetea Lulu.
No comments:
Post a Comment