WADAU WALIA NA KIINGEREZA, UZUNGU KWENYE FILAMU ZA KITANZANIA
Na Mwandishi Wetu
Wadau wa Sanaa
wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia kiingereza kwenye majina ya
filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.
Wakizungumza wiki hii
kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau hao walishangazwa
kitendo cha filamu hizo kutumia majina ya kizungu wakati hapa kwetu kuna filamu
nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.
“Hoja kwamba,
wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto, mbona
hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa
kuna udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora tujikite huko”alisema Mzee
Nkwama Bhallanga.
Kwa mujibu wa wadau
wengi waliozungumza, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na
vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu
maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.
“Maneno kwenye filamu
si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha zaidi, ndiyo maana kuna
watu wanaangalia picha za Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea”
alisema Godfrey Lebejo ambaye ni Murugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na
habari, BASATA.
Aliongeza kuwa,
kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa
tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili
kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni wetu.
“Inawezekana vipi
utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa pamoja kuitazama?
Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye filamu zetu” alionya
Lebejo.
Awali akiwasilisha
mada kuhusu Filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, Msanii wa
filamu Emmanuel Myamba maarufu kam Pastor Myamba alisema kuwa, tasnia ya filamu
inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.
“Ni wazi ukiangalia filamu
zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada, uongozaji, uhariri na hata
uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu huu turekebishe” alisema Myamba
ambaye kwa sasa amefungua kituo cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film
Training Centre (TFTC) kilichoko Ubungo.
No comments:
Post a Comment