Tuesday, June 26, 2012

waandaaji wa Miss Kigamboni watoa vifaa vya ujenzi wa shule

Kutoka kulia ni Mwalimu Mkuu, Colombani Mpogola, Miss Kigamboni wa pili, Agness Goodluck, Mkurugenzi K&L, Angela Msangi na Mratibu Miss Kigamboni, Somoe Ng'itu baada ya makabidhiano ya vifaa vya ujenzi asubuhi ya leo katika shule ya Msingi Kigamboni.

Mratibu wa Miss KIgamboni 2012, Somoe Ng'itu kushoto akiwa na Mkurugenzi wa K&L, Angela Msangi, Miss Kigamboni namba mbili, Agness Goodluck na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigamboni asubuhi hii 
 
Somoe  Ng'itu akisaini kitabu cha wageni katika shule hiyo

Angela Msangi akisaini kitabu cha wageni katika shule hiyo.

WAANDAAJI wa Miss Kigamboni 2012, K&L Media Solutions, asubuhi ya leo wamekabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. Milioni 1.5 kwa uongozi wa Shule ya Msingi Kigamboni, ikiwa ni kutimiza ahadi yao ya kuchangia sehemu ya pato kutokana na shindano lao, lililofanyika Juni 15, mwaka huu katika ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni, Dar es Salaam. 
 
Akikabidhi vifaa hivyo, katika shule hiyo iliyopo mkabala na Mahakama ya Mwanzo ya Kigamboni, Mratibu wa Miss Kigamboni 2012, Somoe Ng’itu alisema kwamba waliahidi kufanya hivyo kwa sababu wanajua umuhimu wa elimu na wanathamini na pia baadhi ya waandajii na warembo wa shindano hilo, walisoma katika shule hiyo. 
 
Somoe, ambaye pia ni Mwandishi wa Habari za Michezo Mwandamizi wa gazeti la Nipashe, alisema kwamba kampuni yao imeamua pia kufanya hivyo ili kutoa mfano kwa wadau wengine kuchangia miradi ya maendeleo ya elimu.Aidha, Somoe ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), alisema kwamba kutimiza ahadi hiyo ni mwanzo tu kwao wa kufanya mambo mengi mengine katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo. 
 
Akipokea misaada hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Colombani Mpogola alisema anawashukuru sana K&L Media Solutions kwa msaada huo, kwani umekuja katika wakati mwafaka na mara moja umeanza kufanyiwa kazi kwa kukarabati baadhi ya madarasa ya shule hiyo. 
 
Mwalimu Mpogola alisema kwamba K&L wametoa mfano mzuri na akawataka wadau na makampuni mengine kuiga mfano huo.Mwanafunzi wa darasa la saba, Sebastian Charles alishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake naye pia akatoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo.
 
Katika shindano la Miss Kigamboni lililofana Juni 15, mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Eddah Sylvester (21) aliibuka mshindi, wakati Agnes Goodluck (20), anayesoma Chuo cha Usimaizi wa Fedha (IFM) mwaka wa pili aliibuka mshindi wa pili na Elizabeth Boniphace (21) aliibuka wa tatu.Washindi hao watatu, na wengine wawili walioingia tano bora, Esther Albert (19) na Khadija Kombo (21) watashiriki shindano la Miss Temeke, Septemba mwaka huu kusaka tiketi ya kushiriki Miss Tanzania Novemba, mwaka huu.  


No comments:

Post a Comment