Wawakilishi Zanzibar: Muarubaini wa kero za Muungano ni kuwa na katiba mpya
Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Wajumbe wa Baraza Wawakilishi Zanzibar
wamesema muarubaini wa kero za Muungano ni kuwa na katiba mpya itakayoweka
bayana mambo yatakayosimamiwa na kila upande kwa uwazi zaidi.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya kudumu ya
kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa makadirio ya mapato na
matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Mwakilishi wa Kwahani(CCM) Ali Salum Haji alisema ikiwa
kutakuwa na katiba itakayobainisha na kuzitambua haki za kila upande wa
Muungano anaamini hakuna nchi itakayomlaumu mwenzie.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo muarubaini wa
matatizo au Kero za Muungano wetu ni kuwa na katiba ambayo itakayobainisha na
kuzitambua haki za kila upande wa Muungano huu na kutofautisha zipi
zitashughulikiwa na kila Nchi katika Muungano huu na zipi zitashughulikiwa na
chombo cha Muungano hapo tunaamini hakuna Nchi itakayo mlaumu mwenzie kama
aidha ni mzigo au anaonewa na mwenziwe” Alisema Mwakilishi huyo.
Mwakilishi huyo aliyewasilisha maoni hayo
kwa niaba ya Mwenyekiti wake, alisema hivi sasa hali haiku hivyo kwani mamlaka
moja imebeba mambo yak wake na ya Muungano ambapo mwengine anahisi kuwa kuna
haki zake za msingi ananyimwa.
“Waheshimiwa Wajumbe sio kama
ilivyo hivi sasa kuwa kuna Mamlaka moja imebeba mambo ya kwake na ya Muungano
ambapo mwingine anahisi kuwa kuna haki zake za msingi ananyimwa na mwenzake, na
hii ndio inayopelekea kuwepo kwa manung’uniko ya kila siku kwa upande mmoja
ambapo yamefikia kupachikwa jina na kuitwa kero za Muungano” Alisema Mwakilishi
Ali.
Mwakilishi huyo alisema katiba ya Jamhuri ya Muungano, Wizara za Muungano ni chache,
lakini kiuhalisia Mawaziri wote
waliopo Tanzania Bara wanafanya kazi zao kama ni Mawaziri wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano.
No comments:
Post a Comment