Wednesday, June 26, 2013

WANAFUNZI WALIOSOMA SHULE ZA KATA VYUO VIKUU WAMTAKA LOWASSA AWANIE URAIS 2015


Mbunge wa Monduli, ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu, Edward Lowasa, akisalimiana na wanafunzi wa chuo kikuu cha UDOM waliotoka shule za sekondari za kata, wakati walipofika nyumbani kwake mkoani Dodoma kutoa shukrani zao kwa hatua waliyofikia kielimu.


Hamida Salum mwanafunzi wa mwaka wa kwanza UDOM, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Mh. Lowasa katikati, Dkt. Mahanga (Kulia) na Parseko Korne wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi hao.
 

WASANII WATAMBA TAMASHA LA FILAMU LA GRAND MALT

Na Mwandishi Wetu
WASANII mbalimbali watakaoshiriki katika Tamasha la Tamasha la Wazi la Filamu Tanzania, maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ ambalo litafanyika katika Viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza, wameanza kutoa tambo zao.
 
Tamasha hilo linatarajiwa kuanza Jumatatu ijayo, ambapo kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya filamu pamoja na burudani za muziki kutoka bendi ya Extra Bongo, pamoja na ngoma za asili.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasanii hao walisema tamasha hilo litawafungua macho wengi ikiwa pamoja na kupata kujua kile ambacho wanakifanya wakati wakirekodi sinema zao.
 
Msanii mahiri wa filamu, Aunty Ezekiel alisema atakuwepo Mwanza kipindi chote cha tamasha hilo na akataka mashabiki wafike kwa wingi kushuhudia filamu kali zaidi ambazo amezicheza katika siku za karibuni, ambazo zitaonyeshwa bure.
 
“Mimi ndiye mkali wao, Watanzania waje kushuhudia kile ambacho tumekifanya,” alisema Aunty Ezekiel, kauli ambayo iliungwa mkono na Jacqueline Wolper aliyedai naye atakuwepo, ila ndiye pia anayejiamini ni ‘mzuri’ zaidi katika mambo ya filamu.
 
Irene Uwoya alitamba atafunika wengi katika tamasha hilo, huku Vicent Kigosi ‘ray’ na Jacob Steven ‘JB’ nao wakijinasibu watafanya vitu adimu zaidi katika tamasha hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi wa filamu hapa nchini.
 
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki alitamba watafanya kweli zaidi siku ya uzinduzi kwani watapiga vibao vipya na kutoa shoo mpya kwa mashabiki watakaojitokeza kipindi chote cha tamasha hilo.
 
“Tumejiandaa vya kutosha, tuna shoo mpya na ya aina yake, ambayo si ya kukosa. Waje tu waone Extra Bongo itakachofanya ni nini,” alisema Choki.
 
Mratibu wa Tamasha hilo aliye pia Mkurugenzi wa Sophia Records, Musa Kissoky, alisema kwa sasa kinachosubiriwa ni siku ya tamasha tu na kusema wasanii wengi wa filamu watakuwepo hapo.
 
“Kwa sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 90, yaani tunaleta kitu tofauti ambacho watu watashangaa, ndio maana mpaka sasa wengi wanapigwa na bumbuwazi kuhusu kile tutakachofanya siku hiyo,” alisema.
 
Naye Meneja wa kinywaji cha Grand Malt walio wadhamini wakuu wa tamasha hilo, Consolata Adam, alisema wameamua kufanya kweli zaidi kwani wanataka kuona Watanzania wanapata kitu chenye uhakika.
 
“Tumejipanga katika hili na wala hatutanii kwani tunataka kuwawezesha wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kuhudhuria tamasha hili kwa wingi . Tunawakaribisha watu wote wenye mapenzi na filamu zetu za Tanzania kufika na kushuhudia tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi,” alisema Consolata.
 
Tamasha la Filamu la Grand Malt linatarajiwa kuanza Julai 1-7, mwaka huu huku kukiwa na filamu mbalimbali zitakazooneshwa katika kipindi hicho. Filamu zote hizo ni kutoka Tanzania.
 
Tamasha hilo la filamu limedhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi ambacho kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana vyema na ISAMILO LODGE ya Mwanza.

No comments:

Post a Comment