Wednesday, June 26, 2013

BALOZI IDDI AZINDUA JENGO LA SKULI YA MIWANI JIMBO LA UZINI UNGUJA

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana ana Wanafunzi wa Skuli ya Msingi wa Miwani, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa jengo lao jipya. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akilizindua rasmi jengo jipya la madarasa mawili ya Skuli ya Msingi ya Miwani iliyomo ndani ya Jimbo la Uzini.
 Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza akimpatia maelezo ya ujenzi wa Jengo la Skuli ya Msingi ya Miwani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kulizindua rasmi.
Balozi Seif akimpongeza Msaidizi Mkurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar  { PBZ } Ame Haji Makame kwa hatua ya benki hiyo kusaidia vikalio kwenye jengo jipya la skuli ya msingi ya miwani. Kulia yao ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza Hassan na Pembeni yao Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Dr. Islamu Idriss.
*********************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema  wakati umefika kwa Wananchi kuwa na hadhari katika kuangalia Mtu mwenye muelekeo wa kuwafaa katika kuwasimamia kusukuma mbele maendeleo yao wanayoyahitaji kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizindua rasmi jengo jipya na la kisasa la Skuli ya Msingi  ya Miwani ndani ya Jimbo la Uzini lililojengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd Raza Hassan.
Balozi Seif alisema ile tabia ya baadhi ya wananchi kukumbatia watu wanaoendeleza ubinafsi inafaa kupigwa vita kwa hali yoyote ile kwa vile inachangia kuzorotesha kasi ya Maendeleo ya Wananachi.
Aliwahimiza Viongozi, washirika na wahisani zikiwemo Taasisi za Kijamii na zile za maendeleo zilizomo katika Halmashauri za Wilaya kujikita zaidi katika kuunga mkono juhudi za Wananachi kwenye sekta za Mendeleo na Kiuchumi wakiangalia zaidi ile sekta muhimu ya Elimu.
“ Siku zote tunasema tuwekeze kwenye elimu ambayo watoto wetu itawasaidia wao wenyewe kwa kupata muelekeo na mafanikio ya maisha yao sambamba na kusaidia familia zinazowazunguuka “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza kwa hatua yake aliyochukuwa ya ujenzi wa Jengo hilo la madarasa mawili lililokamilika huduma zote ikiwemo vikalio ambalo limesaidia kuiepusha Skuli ya Miwani kuchukuwa wanafunzi katika mikondo miwili.
Balozi Seif alisema juhudi za Mwakilishi huyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ya CCM pamoja na kukamilisha ahadi alizotowa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo hilo.
Aliwakumbusha Viongozi wengine wa Jimbo, Wilaya na hata mkoa kuunga mkono jitihada za Wananachi wa Miwani katika kukamilisha jengo jengine la Madarasa  Sita la Skuli hiyo ambalo linahitaji nguvu za ziada za Viongozi hao likiwa limekwama kwa  miaka minne sasa.
Alisema katika kuunga mkono juhudi hizo za Wananchi ambapo zinahitajika kiasi cha shilingi Milioni Tisa { 9,000,000/- } kukamilisha hatua ya linta ili likabidhiwe  Wizara ya Elimu  na Mafunzo ya Amali kwa Ukamilishaji aliahidi kuchangia Shilingi Milioni Mbili { 2,000,000/- }.
“ Sisi viongozi kuanzia Wawakilishi wa kuteuliwa, Mbunge, Madiwani na hata halmashauri za Wilaya tunalazimika kuunga mkono juhudi hizi ili kutowavunja moyo wananchi tunaowaongoza katika Majimbo yetu “. Alikumbusha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa salamu za Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } iliyosaidia Vikalio vyote vya jengo hilo Meza 100 na Viti 100 vyenye thamani ya shilingi Milioni 16,000,000/-  Msaidizi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki  hiyo  Ame Haji Makame amesema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Wananchi popote pale.
Nd. Ame alisema benki ya Watu wa Zanzibar inajali maendeleo ya Jamii na wakati mwengine kushawishika kusaidia miradi yao tofauti ikiwemo zaidi sekta ya elimu ambayo ndio mkombozi wa Taifa lolote.
Naye kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Mwanaidi Saleh amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Raza kwa juhudi zake za kusaidia nguvu za Wizara hiyo katika ukamilishaji wa majengo  ya Skuli.
Bibi Mwanaidi alisema juhudi za Mwakilishi huyo za kukamilisha majengo mawili ya Skuli ndani ya Jimbo hilo limeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya Elimu wa kukamilisha majengo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wizara hiyo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu amewakumbusha Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini kuhakikisha kwamba majengo ya skuli wanayoyaanzisha yanatengewa vyumba maalum kwa ajili ya vitengo vya Kompyuta.
Alisema Wizara imeanzisha mfumo maalum wa mafunzo ya kompyuta kuanzia elimu ya msingi kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia yaliyopo Duniani.
Akitoa shukrani zake katika hafla hiyo ya uzinduzi wa jengo jipya la Skuli ya Miwani iliyomo ndani ya Jimbo la Uzini Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd Raza Hassan alisema kwamba uwepo wa Viongozi katika Jamii upo kwa ajili ya kusimamia matakwa ya Wananchi.
Mh. Raza alisema tabia ya baadhi ya Viongozi kuigonganisha vichwa jamii ni kutowafanyia haki Wananachi wanaowaongoza na hatimae inaviza maendeleo yao na kuwaongezea chuki na fitna baina yao.
Mapema katika Risala yao iliyosomwa na Mwalimu  wa Skuli ya Msingi ya Miwani Juma Abdulla wananchi hao wa Kijiji cha Miwani walisema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ndani ya Kijiji hicho.
Mwalimu Juma alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa bara bara, mashine za uchapaji , ukosefu wa Daktari katika kituo chao cha Afya pamoja na umaliziaji wa jengo lao la madarasa sita ambalo linaweza kusaidia muendelezo wa mkondo mmoja tu skulini hapo.
Jengo jipya  la  madarasa mawili la Skuli ya Msingi ya Miwani litakalokuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 122 ambapo wanafunzi  56 kwa kila chumba  lilijengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili kwa gharama za shilingi Milioni 30,000,000/- .
Katika hafla hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Uzini pia alikabidhi Mchango wa Shilingi Milioni Mbili kwa ajili ya Kusaidia maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi Mtukufu ya Zanzibar hapo mwaka 2014.
Fedha hizo zitasaidia katika Ofisi ya Mkoa Kusini Unguja, Wilaya ya Kati, Jimbo la Uzini Kichama pamoja na kukabidhi pia mipira kwa ajili ya Timu za Skuli 12 zilizomo ndani ya Jimbo la Uzini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/6/2013.

No comments:

Post a Comment