Wednesday, June 19, 2013

*SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA ARUSHA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetuma salamu za rambi rambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Magesa Mwilongo kutokana na vifo vya wananchi watatu wa Mkoa huo vilivyotokea kufuatia mlipuko wa bomu uliotokea  mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Soweto Jijini Arusha.

Watu wasiopungua 70 waliripotiwa kujeruhiwa  wakati wa mripuko huo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi katika Kata ya Soweto  wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo { Chadema }.

Katika Taarifa ya rambi rambi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  iliyotumwa kwa Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha  na kutiwa saini na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea kupokea kwa masikitiko na huzuni taarifa ya shambulio la kigaidi la bomu lililotokea tarehe 15 Juni mwaka 2013.

Balozi Seif alisema Taifa kwa mara nyengine tena limekumbwa na msiba wa njama za kigaidi zilizoua na kujeruhi raia wema wasio na hatia sambamba na tukio jengine linalofanana na hilo lililogharimu roho za wananchi wengine wakati wakiwa katika ibada Kanisani.

Balozi Seif alisema kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wananchi na yeye binafsi anatuma salamu hizo za rambi rambi kutokana na maafa hayo na kuwaombea marehemu malazi pema na majeruhi wapone haraka ili waungane na wenzao katika ujenzi wa Taifa.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaiunga mkono Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kupambana na ugaidi wa aina yoyote hapa Nchini.

Alieleza kwamba SMZ na Wananchi wa Zanzibar wako pamoja na wenzao katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na maombolezo na kuwaomba wafiwa wawe na moyo wa ustahamilivu, uvumilivu na subra katika kipindi hichi.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kutenga shilingi Milioni Mia Moja { 100,000,000/-} kama zawadi kwa kwa mtu ye yote atakayetoa Taarifa zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu au watu wenye mtandao wa ulipuaji wa mabomu hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/6/2013.

No comments:

Post a Comment