Wednesday, June 26, 2013

RAIS WA TFF LEODGER TENGA WATAKA MAKOCHA WALIOMALIZA KOZI KUIBUA VIPAJI VYA SOKA NCHINI

Mhitimu wa kozi ya ukocha wa mpira wa miguu kwa ngazi ya pili, Seleman Matola akipongezwa na Rais wa Shirikisho la Soka nchini, Leodgar Tenga kwenye sherehe zilizofanyika Uwanja wa Taifa. Kulia ni Mwenyekiti wa DRFA Almas Kassongo na (kushoto) Mkurungenzi wa Ufundi TFF, Sunday Kayuni.
***********************************
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodger Tenga, amewataka makocha kuhakikisha wanaibua vipaji vya watoto ili kuwa na vipaji vingi baadaye.
Tenga alikuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa kozi hiyo ya ngazi ya pili  iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kozi hiyo iliyoendeshwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa Dar es Salaam (DRFA), ilianza Juni 3 huku ikishirikisha zaidi ya makocha 58.
Tenga alisema Bara la Afrika ndilo bara lenye upungufu mkubwa wa wachezaji watoto, tofauti na mabara mengine, kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya soka.
“Hili ndilo bara ambalo lipo nyuma katika kuibua vipaji, mfano nchi ya Ujerumani pekee ina watoto zaidi ya milioni  moja ambao wanaandaliwa, lakini hapa sijui kama wanafika hata idadi hiyo, hivyo kuna changamoto kubwa katika hilo,” alisema.
Aliwataka kuhakikisha wanayatumia mafunzo hayo katika kuleta mabadiliko katika soka hapa nchini, ambapo pia aliwapongeza kwa kushiriki katika kozi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kassongo amesema kozi hiyo itakuwa mkombozi wa makocha kusaidia timu zao kufanya vizuri na kuendeleza mchezo huo nchini.
"Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa TFF kwa kukubali kuwa nasi licha ya majukumu mengi aliyonayo, lakini niseme tu kwamba kozi hii imekuwa ya mafanikio kutokana na kushirikisha wachezaji wengi wa zamani," alisema.
Baadhi ya washiriki waliohitimu kozi hiyo ni pamoja na Moses Mkandawile, Shedrack Nsajigwa, Ibrahim Masoud Maestro, Shaffih Dauda, Rahel Pallangyo, Ally Yusuph Tigana, Emanuel Gabriel, Jemedari Said, Benard Mwalala, Edibily Lunyamila, Seleman Matola na wengineo.

TANZANIA YASHINDA TUZO 3 ZA UTUMISHI WA UMMA BARANI AFRIKA NCHINI GHANA.

 
Tanzania imeshinda tuzo tatu za juu za ubunifu katika Utumishi wa Umma, barani Afrika, kufuatia Tasisi tatu za Tanzania, kushinda nafasi ya kwanza, na kukabidhiwa vikombe vya ushindi na rais wa Ghana, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma barani Afrika, yaliyofanyika jana mjini Accra nchini Ghana.
Taasisi za Tanzania zilizoshinda ni Ofisi ya  Ukaguzi ya Taifa, (NAO), Wakala wa Vipimo, (WMA),  na Wakala wa Vitambulisho vya Taifa, (NIDA) kufuatia kufanya vizuri katika maonyesho ya  siku 7 ya shughuli mbalimbali za utumishi wa umma yaliyofikia kilele tarehe 23/06/2013.
Akiuzungumzia ushindi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Celina Kombani, amezipongeza taasisi hizo, zilizolitea sifa taifa hili na kuelezea kufarijika kwake na ushiriki wa  mkubwa wa Tasisi za Tanzania katika maonyesho hayo ambapo jumla ya taasisi 42 kutoka Tanzania, zilishiri.
Akisoma hotuba katika kilele cha maandimisho hayo, Mhe. Kombani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Utumishi Barani Afrika, amewataka watumishi wa umma kote barani Afrika, kuwatumikia wananchi kwa  bidii,
unyenyekevu, uadilifu wa hali ya juu, na kueleza utumishi wa umma ni kuwatumikia watu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Gearge Yambesi, amekiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri sana katika utumishi wa umma barani Afrika, hali inayofanya Tanzania kujijengea heshima kubwa barani Afrika na Ulimwenguni kwa ujumla.
Wakizungumzia kuhusu ushiriki wa Tanzania katika maonyesho hayo, Waziri , Mhe. Celina Kombani,  na Katibu Mkuu, Bwana. George Yambesi, wanaeleza zaidi.
Akizungumzia maonyesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Press and Public Relations (PPR), Bw. Pascal Mayualla, amesema mfulululizo wa vipindi vya redio na Televisheni, kuhusu ushiriki wa Tanzania, katika Maonyesho ya Utumishi wa Umma barani Afrika, vitaanza kuonekane kesho, katika vituo mbalimbali vya redio na Televisheni. 
 

WANAWAKE WANA UWEZO WA KUBADILISHA MAISHA YA MTANZANIA

Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa akitoa hotuba yake  wakati wa ufunguzi  wa mafunzo ya siku tatu ya wanawake wajasiriamali yanayoendelea kwenye  ukumbi wa Bwalo la Maafisa la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Mgulani jijini Dar es salaam.
***************************************
WANAWAKE wakiwezeshwa kiuchumi na kupatiwa elimu ya msingi ya ujasiriamali, kuepuka maradhi hatarishi na kufahamu haki zao katika jamii, umasikini utapungua,  kipato  kitaongezeka na maisha ya Watanzania yatabadilika. 
 Hayo  yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa wakati wa ufunguzi  wa mafunzo ya siku tatu ya  wanawake wajasiriamali yanayoendelea kwenye  ukumbi wa Bwalo la Maafisa la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Mgulani jijini Dar es salaam.

Mama Anna Mkapa ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa   alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii  wajasiriamali  hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani, ambapo jumla ya wanawake wapatao 264 wanashiriki.

“Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote umekusudia kwa nguvu zake zote kuendeleza vita ya hii ya kuwawezesha wanawake  nchini  kujikwamua katika wimbi la umasikini, maradhi na ujinga,” alisisitiza Mama Mkapa.
 Aidha ameiomba Serikali, Asasi za kiraia, taasisi za dini, wahisani binfasi ndani na nje ya nchi, kusaidia  wanawke haswa wa vijijini   kujikwamua na umasikini. 

 Mama Mkapa  aliongeza  kuwa mfuko huo, kwa kipindi cha miaka 16  zaidi ya wanawake 6,820 wamepata mafunzo ya stadi za biashara na wengine  4,500 wamepata fursa ya kushiriki maonyesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa kupitia EOTF ili  kutangaza na kuuza bidhaa zao.

 Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Dk. Abdallah Kigoda  akifungua mafunzo hayo alisema  Serikali imeanzisha utaratibu wa kuweka kumbukumbu za mkopo katika mabenki kwa kupitia ‘Credit Reference Bureau’ ili kuweza kusaidia kuwafahamu wateja, na kuwaasa wajasiriamali wanapokopa wakumbuke kulipa kwani uaminifu ni kitu muhimu katika biashara.
“Suala lingine la kulipa kipaumbele ni lile la kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha na tuache kuwazalishia watu wengine bidhaa wakaenda  kuongezea thamani kidogo tu kama vile kwa kufunga na kuweka nembo ya kibiashara na kuuza kwa bei kubwa,” alisema Dk. Kigoda. 
Aliahidi kuwa Wizara yake iko makini kufanya linalowezekana kushirikiana na wajasiliamali hao kutatua  tatizo hilo la kuuza malighafi badala ya bidhaa iliyoongezwa thamani  ili kuongeza ajira na kupunguza umasikini.

No comments:

Post a Comment