Monday, June 24, 2013

ABDUKIBA AJA NA 'SIAMINI'


MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abdukarim Kiba ‘Abdukiba’ yuko mbioni kuachia kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Siamini’ hivi karibuni.

Akizungumzia kibao hicho, Abdukiba alisema, yupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa wimbo huo na ataisambaza katika vituo mbalimbali vya radio mwishoni mwa wiki hii.

Alisema katika wimbo huo, kuna baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya watasikika, ambao hajapenda kuwataja ili kuwapa mtihani mashabiki wake kujiuliza nani ambaye kamshirikisha.

“Sipendi kusema nimemshirikisha nani katika wimbo huo, ila ningependa mashabiki wangu wakae mkao wa kula kwa ajili ya wimbo huo, najua wengi wataupenda kulingana na jinsi ulivyo tofauti na nyimbo nyingine,” alisema Abdukiba.


Mbali na ‘Siamini’, Abdukiba alishawahi tamba na vibao kama ‘Kizunguzungu’, ‘Huyo si demu’ ‘Kidela’ na nyinginezo ambazo zinafanya vizuri katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya.

MATONYA 'ANAJIAMINI'



MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Seif Shabani ‘Matonya’ amesema yupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Najiamini’.

Matonya kwa sasa anatamba na kibao ‘Zilipendwa’ ambacho kinafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kutokana na maudhui yaliyopp ndani yake.

Aliwaomba mashabiki wake wakae mkao wa kula kwa ajili ya kukipokea kibao hicho ambacho anaamini kitafanya vizuri.

“Mashabiki wangu wananijua kwamba nipo kamili na huwa sitoi vitu ambavyo havijakamilika, naomba wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuipokea kazi hiyo ambayo itakuja pamoja na video yake,” alisema.

Mbali na kazi hizo, mkali huyo alishawahi kutamba na vibao vyake kama, ‘Taxi Bubu’, ‘Violeth’ na vinginezo ambavyo vilimtambulisha katika tasnia ya muziki wa bongo fleva.

'MUSIC' YA STEVE RNB YAANZA KUTESA



WAKATI singo yake ya ‘Jambo Jambo’ ‘ikiendelea kufanya vema katika chati mbalimbali za muziki nchini, mkali wa muziki wa bongo fleva, ‘Steve RnB’ ameachia singo mpya inayokwenda kwa jina la ‘Music’, ambayo pia imeanza kutamba katika tasnia hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mkali huyo alisema ameamua kutoa singo hiyo mpya ili kuendelea kuwapa raha mashabiki wake ambao wamekuwa wakimuunga mkono.

Alisema anayo matumaini makubwa ya wimbo huo kufanya vema katika medani ya muziki wa bongo fleva kama ilivyokuwa kwenye nyimbo zake zilizotangulia.

“Nawashukuru mashabiki kwa kuniunga mkono kwenye kazi zangu, sina cha kuwalipa zaidi ya kuwatayarishia kazi nzuri zaidi ambazo zitawaburudisha na kuwapa mafunzo ndani yake,” alisema.

Steve alipata kutoa singo matata ikiwamo ya ‘One Love’ alioimba na Baby Boy na nyinginezo ambazo zilimtambulisha na kufanya vizuri katika tasnia ya muziki huo.

No comments:

Post a Comment