Tuesday, June 26, 2012

JOKETI AENDESHA MNADA WA KONDOO WA AMANI


Mbunifu wa mitindo nchini, Jokate Mwegelo juzi aliendesha mnada wa Kondoo wa amani maalum kupinga matukio ya kuhatarisha amani yaliyotokea Zanzibar hivi karibuni.
Mnada huo uliandaliwa na kikundi cha wanamichezo cha Taifa Jogging kwa kushirikiana na wageni wao kutoka  Zanzibar wajulikanao kwa jina la Kitambi Noma.
Mbali ya kufanya mazoezi, wanamichezo hao walikusanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja chini ya mgeni Rasmi, Kanali Mstaafu na mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Idd Kipingu ambaye aliwapongeza waandaaji wa shughuli hiyo kwa kuhamasisha amani nchini.
Kipingu alisema kuwa amani ndiyo silaha pekee kwa sekta zote pamoja na michezo kwani kutokuwepo kwake hakuna kitakaochofanyika katika jamii.
Alisema kuwa kilichofanyika kwa wanamichezo hao ni mfano wa kuigwa na kuwataka wanamichezo nchini kupigania amani mbali ya kushiriki katika michezo tofauti.
Katika Mnada huo, Jokate ambaye kwa sasa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya ubinifu wa mitindi ya Kidoti aliweza kumuuza kondoo huyo kwa sh. 200,000 kutoka kwa wanamichezo hao.
Mrembo huyo wa zamani alisema kuwa baada ya kumuuza kondoo huyo, aliondoka na kundi la Kitambi Noma na kwenda Zanzibar ambako atachinjwa na kuliwa kama ishara ya kudumisha amani.
“Nimefarijika sana kwa kushiriki katika mnada huu, mwaliko wangu umetokana na jinsi gani ninavyojishughulisha katika masuala mbali mbali ya Jamii, mbali ya mitindo au kama mmoja wa warembo waliofanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania,” alisema.

No comments:

Post a Comment