Tuesday, June 26, 2012

Chama cha wafanyakazi ATCL chaahidi kutoa ushirikiano kwa menejimenti mpya ili kuendeleza ufanisi wa shirika hilo

CHAMA cha wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) kimekanusha vikali taarifa mbalimbali zinazohusisha chama hicho na kupinga mabadiliko ya uongozi katika shirika hilo yaliyofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dkt Harrison Mwakyembe, wiki chache zilizopita na kusema kuwa taarifa hizo hazina ukweli ndani yake.

Dkt. Harrison Mwakyembe alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Bw. Paul Chizi na kumteua rubani wa siku nyingi Kapteni Milton Lazaro na kusema kuwa uteuzi wa Bw. Chizi haukufuata taratibu zilizosahihi.

Mwakyembe alipokuwa akihutubia mkutano wa wafanyakazi wa ATCL katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam siku moja baada ya kutangaza mabadiliko hayo ya uongozi, aliwaamuru wafanyakazi wa ATCL ambao hawakuridhika na uteuzi wa Kapteni Lazaro kujiuzuru maramoja. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Gerald Msuya jijini Dar es Salaam jana, alisema kuwa chama icho kitatoa ushirikiano mzuri kwa uongozi mpya uliyoingia madarakanii ili kuhakikisha shirika linazidi kusonga mbele.

“Chama cha Wafanyakazi ATCL akina taarifa zozote kuhusiana na habari hizo zinazotolewa na vyombo vya habari kuhusu kupinga uteuzi wa Waziri. Tunauheshimu uteuzi wa Dkt. Mwakyembe na tutatoa ushirikiano kadri iwezekanavyo kuhakikisha shirika letu linazidi kusonga mbele,” alisema. Aidha, alisema kuwa taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari ni taarifa zisizonaukweli wowote zinazotolewa na watu wenye chuki binafsi ndani ya shirika ambao hawataki  kuona shirika hilo kujikita katika masuala ya msingi ya maendeleo kibiashara.

“Taarifa hizi kawaida zimekuwa hazina vyanzo vinavyoaminika. Kama wanatoa taarifa za ukweli, kwanini wanaficha majina yao?” “Chama cha Wafanyakazi ATCL kinaongozwa na katiba ambayo inaelekeza taratibu rasmi za kufuata na kufikisha malalamiko kwa ngazi zinazostahili lakini cha kushangaza hatujapata malalamiko yoyote mbali na kuona malalamiko yasiyorasmi kwenye vyombo vya habari,” alisema Msuya.

Hata hivyo, Msuya alisema kuwa chama chake kitafanya uchunguzi wa kina ili kuwatambua watu hao wanaotoa taarifa hizo potofu na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitafuatwa kwa watakaobainika kutoa taarifa hizo ili kutoa onyo kwa wengine .  “Tunahitaji kuelekeza juhudi zetu katika masuala ya msingi baada ya kupoteza muda na kutoa taarifa potofu kwa baadhi ya watu wenye ubinafsi, na tunatoa shukrani zetu maalum kwa serikali yetu kwa kuonyesha imani na sisi tena na tunaahidi hatutawaangusha,” alisema.

No comments:

Post a Comment