Thursday, October 4, 2012

SIR NATURE KUPAGAWISHA ROCK CITY MARATHON 2012

Msanii maarufu wa Bongo Flava, Juma Kassim ‘Sir Nature’ (katikati), akiimba mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kibao chake kipya cha ‘Narudi kijijini’ alichomshirikisha Baby Madaha (kulia). Nature atazindua kibao hicho Oktoba 28, wakati wa mbio za Rock City Marathon 2012 zitakazofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kiruma jijini Mwanza. Kushoto ni Mratibu wa Rock City Marathon, Grace Sanga. 
DAR ES SALAAM, Tanzania
 
“Nitatoa burudani safi kwa mashabiki na wanariadha wenyewe watakaoshiriki Rock City Marathon 2012 jijini Mwanza. Wakazi wote wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, wategemee burudani kali na nawataka wajitokeze kwa wingi kushiriki Rock City Marathon”

NYOTA muziki wa Bongo Flava, Juma Kassim ‘Sir Nature,’ leo ametamba kufanya shoo ya aina yake na kuwapagawisha mashabiki na washiriki wa mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazofanyika Oktoba 28 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sir Nature amesema yeye na kundi lake la Wanaume Halisi wamejipanga kikamilifu, kuhakikisha wanakata kiu ya kila shabiki na mshiriki wa mbio hizo zilizo chini ya Uratibu wa Capital Plus International.

“Nitatoa burudani safi kwa mashabiki na wanariadha wenyewe watakaoshiriki Rock City Marathon 2012 jijini Mwanza. Wakazi wote wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, wategemee burudani kali na nawataka wajitokeze kwa wingi kushiriki Rock City Marathon.

“Kwa kuwa michezo ni afya, nategemea wakazi wengi wa Mwanza na vitongoji vyake watatumia muda uliobaki kujisajili ili wawe sehemu ya tukio hilo muhimu maishani litakalofanyika Oktoba 28, ndani ya dimba la CCM Kirumba,” aliongeza Sir Nature.

Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo Grace Sanga wa Kampuni ya Capital Plus International (CPI), alisema kuwa maandalizi yanaendela vizuri huku akisema mbio za mwaka huu zimeboreshwa zaidi ukilinganisha na za mwaka jana.

“Maandalizi yanaendelea vizuri na natumia nafasi hii kuomba wananchi ambao mpaka sasa hawajajitokeza kusajiliwa, kufanya hivyo haraka kuwahi muda na nafasi zilizosalia. Natumia nafasi hii pia kutoa shukrani kwa wadhamini wetu kwa kutuunga mkono,” alisema Grace.

Rock City Marathon 2012 ni mbio hizo zilizo chini ya udhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Airtel Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottles, PPF, Geita Gold Mine, TANAPA, Sahara Communication, ATCL, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.

Aidha, Grace aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuchukua fomu za usajili kwenye Ofisi za Uwanja wa Nyamagana Mwanza, Ofisi za Capital Plus International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, Ofisi za Bodi ya Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar es Salaam, pia kupitia tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment