Saturday, July 28, 2012


Meli ya Mv Skagit ikizama.

Ikiwa ni siku tisa tu toka kutokea kwa ajali ya Mv Skagit iliyochukua maisha ya Watanzania zaidi ya 80, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na mipango ya maendeleo kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani ya wiki moja kutoka sasa  kwa ajili ya kununua meli kubwa mpya ya abiria elfu moja na yenye uwezo wa kubeba mizigo ya tani 100.

Ametoa hilo agizo wakati akizungumza na uongozi wa shirika la meli pamoja na wajumbe wa bodi ya shirika hilo ambapo ameagiza wizara kutafuta hizo pesa kutoka kwa vianzio vya ndani au nje ya Nchi vilevile taasisi zinazohusiana na mambo ya fedha.

Huu ni mfano wa meli yenye uwezo wa kubeba abiria 1000.

Dr Shein amesema katika kipindi kisichozidi miezi miwili anahitaji ujumbe maalum uende kwenye kampuni zinazotengeneza meli Korea Kusini, China au Japan kwa ajili ya kuwasilisha fedha za utangulizi kwa ajili ya ujenzi wa hiyo meli.

Baada ya kusema hayo, Uongozi wa shirika la Meli ulimueleza kwamba kwa kawaida ujenzi wa meli yenye ukubwa huo huchukua mwaka mmoja kukamilika.

Kikao hicho kilikua na lengo la kuangalia mwelekeo na mipango ya shirika la meli pia, kilijadili hali ya meli za shirika la meli na baadae kujadili masuala ya ununuzi wa meli mpya itakayoondoa usumbufu wa usafiri wa baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania bara.

No comments:

Post a Comment