Tuesday, July 17, 2012

Waziri atishiwa kuuawa


Wakati  taifa likiwa katika hisia za kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, amepokea vitisho vya kuuawa.


Lengo la vitisho hivyo inaelezwa kuwa ni kufifisha mpango wa bomoa bomoa ya nyumba zilizojengwa kinyume na Sheria ya Mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa, Dk. Huvisa alisema baada ya kutangaza (kupitia bungeni), kuhusu bomoa bomoa, mtu asiyejulikana alimpigia simu na kumtishia kumuua, ikiwa utekelezaji wake utafanyika.

Alipohojiwa na NIPASHE, Dk. Huvisa alisema mtu aliyemtishia alimpigia simu na kusema: “Wewe unajifanya kuwa kinara wa kutaka kubomoa nyumba zetu, elewa kuwa ukifanikisha nia hiyo tunakuua.”

Vitisho hivyo vimetolewa ikiwa ni siku chache tu tangu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa kushirikiana na Wizara za Maliasili na Utalii na ile ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilibomoa nyumba 17 na kuta nane za uzio zilizojengwa kwenye maeneo ya fukwe za Mbezi na Kawe jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Huvisa, bomoa bomoa hiyo iligharimu Sh. milioni 50 ambazo zitawasilishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, ili zilipwe na watu waliobomolewa nyumba zao.

Dk. Huvisa alisema baada ya kupokea vitisho hivyo kwa njia ya simu, alijaribu kumpigia mhusika mara kadhaa, lakini simu yake haikupokelewa.

Alisema kwa hali hiyo, alishindwa kuchukua mchakato wa kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi, lakini aliwaonya wanaoshiriki kutoa vitisho hivyo.

“Niliamua kumpuuzia na sikuona sababu ya kwenda kutoa taarifa bungeni, kwa sababu ningemshitaki nani?,” Alihoji.

Pia, Dk. Huvisa alisema Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), ambaye hakumtaja kwa jina, alitishiwa kwa njia ya simu na kutoa taarifa polisi.

Pamoja na kutomtaja kwa jina Mwanasheria huyo, Dk. Huvisa ambaye hakutaja kituo cha polisi ambapo taarifa hiyo ilitolewa, alisema tukio hilo liliwasilishwa kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

BOMOABOMOA YAJA NCHI NZIMA

Dk. Huvisa alisema bomoabomoa ya nyumba za makazi na biashara zilizojengwa kwenye maeneo ya fukwe za bahari na maziwa na kando kando mwa mito na mabwawa, kinyume cha Sheria ya Mazingira inatarajiwa kuendelea nchi nzima.

Bomoa bomoa hiyo itazihusisha nyumba na shughuli za binadamu zilizojengwa na kufanyika katika maeneo yenye vyanzo vya maji na misitu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, ujenzi na uendelezaji wa shughuli za binadamu unapaswa kufanyika eneo lililopo umbali wa kuanzia mita 60 kutoka pigo la mwisho la mawimbi.

Alisema watu watakaohusika katika bomoa bomoa hiyo watatakiwa kulipa gharama za ubomoaji, isipokuwa wale waliothibitishwa kujenga na kuendeleza maeneo yao kabla ya kuwepo kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Dk. Huvisa alisema bomoa bomoa hiyo ina changamoto zinazoifanya kuwa ngumu, hivyo kulazimisha ushirikishwaji wa wizara nyingine kama za maliasili na utalii na ile ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi.

Alisema wapo wamiliki wa nyumba wenye vibali kutoka kwa mamlaka husika ambazo tathimini ilifanyika na kukubaliwa kulipwa fidia na waliohusika kutoa vibali, lakini wasiokuwa kwenye kundi hilo hawatalipwa, isipokuwa kufidia gharama za ubomoaji. 

KASORO ZA UJENZI WA HOTELI FUKWENI

Dk. Huvisa alisema kuna kasoro kadhaa katika ujenzi wa hoteli kwenye fukwe za bahari, lakini ubomoaji wake utaligharimu taifa fedha nyingi. 

Alitoa mfano wa kasoro hizo kuwa ni ujenzi ulio karibu na fukwe ambao ni tofauti na nchi zilizofanikiwa kutunza fukwe zao kama Brazil panapofanyika mikutano ya kimataifa ya maendeleo na mazingira. 

“Hatuwezi kuzibomoa hoteli zilizojengwa kisheria ingawa zipo karibu sana na fukwe, isipokuwa kinachotakiwa sasa ni kuyaokoa maeneo ya fukwe ambayo hayaguswa kwa ujenzi huo,” alisema.

Kumekuwepo taarifa za ujenzi holela wa hoteli zilizopo ufukweni hususani katika ukanda wa pwani wa bahari ya Hindi na visiwa vya Zanzibar.

Huyu anakuwa Waziri wa tatu kutishiwa kuuawa kutokana na utendaji wa kazi, ambapo awali Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alitishiwa kuuawa.

Baada ya vitisho hivyo, Februari 8, mwaka jana Dk. Mwakyembe alikwenda Polisi kuzungumza na IGP ambaye alimtaka kuweka kwenye maandishi madai hayo naye aliyawasilisha kwa maandishi siku iliyofuata.

Hata hivyo, hakuna mtu ambaye amekamatwa kutokana na taarifa hizo na kumekuwa na taarifa za Dk. Mwakyembe kulishwa sumu kwa nia ya kuuawa. Dk. Mwakyembe alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu baada ya kupata ugonjwa wa mparanganyiko wa ngozi uliopelekea kunyonyoka nywele zote na ngozi kutoka magamba.

Kadhalika, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliwahi kutishiwa kuuawa baada ya kuendesha zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam.

NIPASHE ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senzo, lakini mara zote simu yake ya mkononi iliita bila majibu wakati ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, hakupatikana.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa na NIPASHE kuhusu vitisho hivyo, alisema hakuwa na taarifa.

"Sina habari hizo lakini nikipata details za kutosha tutazishughulikia tena haraka, ni vyema Waziri akaeleza alikotoa taarifa ili kama ni hapa (Dar), nifuatilie uchunguzi wake," alisema.

No comments:

Post a Comment