Friday, August 10, 2012


Profesa Mahalu akiongea na waandishi wa habari baada ya ushindi. 

Baada ya kesi yake kuendeshwa kwa miaka sita kuhusu ishu ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya euro milioni mbili, hatimae Mahakama ya hakimu mkazi kisutu imewaachia huru watuhumiwa ambao ni balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu pamoja na ofisa utawala wa ubalozi huo Grace Martin.

Baadhi ya waliotoa ushahidi kwa upande wa washtakiwa ni pamoja na rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na watuhumiwa kudaiwa kuwa na baraka za ikulu wakati huo wa uongozi wa Mkapa.

Hakimu wa Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Ilvin Mgeta amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka umeshindwa kuwatia hatiani watuhumiwa hao.

Katika kesi hiyo ambayo jumla ya mashahidi kumi walitoa ushahidi wakiwemo watatu wa upande wa washtakiwa na saba kwa upande wa mlalamikaji, Prof Mahalu na Grace Martin walikua wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya euro milioni mbili wakati wa ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Baada ya hakimu kutoa kauli ya mwisho, Watuhumiwa hao walipata nafasi ya kuzungumza ambapo Profesa Mahalu alisema “Mungu amedhihirisha utukufu wake, kwamba Mungu siku zote hutetea wanyonge na mimi kila wakati nilikua nikisoma Warumi 8 mstari wa 31, Mungu akiwa na wewe hakuna atakaekua dhidi yako”
Grace Martin alisema “Namshukuru mwenyezi Mungu kwa wema mkuu alionionyesha kwa miaka hii yote sita, Mungu wangu ni mwaminifu sana”

No comments:

Post a Comment