VIONGOZI WA SERIKALI, DINI, VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUHUBIRI AMANI MAJUKWAANI
VIONGOZI
wa Serikali, Dini na Vyama vya Siasa nchini wametakiwa kuondoa tofauti
zao na kutumia majukwaa kuhubiri amani na upendo ili kudumisha
mshikamano na utulivu ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa hivi
karibuni na Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini
Magharibi Ushirika wa Itiri Daniel Siame wakati wa ibada ya mazishi ya
Ditective Sagenti Christopher Kyendesya aliyefariki Juni 19 mwaka huu
wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa ajali ya Pikipiki.
Mchungaji Siame alisema kuwa
Serikali haina dini bali jamii ndiyo inadini mbalimbali zikiwemo za
Ukristo, Uislamu na Upagani na kuwaomba viongozi hao pale wanapokutana
na wananchi kuhubiri mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Inawezekana kuwa ndani ya
dini zetu kuna watu ambao wanamapokeo ya dini tu na siyo kumtangaza
Mwenyezi Mungu hivyo basi sisi kama viongozi wa Serikali, Dini na Vyama
vya siasa tunakazi kubwa ya kutangaza mambo ya kumpendeza Mwenyezi Mungu
na amani na siyo mambo ya uchochezi”, alisema Mchungaji Siame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Mbeya Abbas Kandoro alimshukuru mchungaji huyo kwa kuwahimiza watu
wote wakiwemo viongozi na wananchi kuhusu umuhimu wa amani na upendo
katika jamii.
Kandoro alisema kuwa ni jukumu
lao viongozi wa Serikali, Dini na wanasiasa kutumia lugha ya kuwajenga
watanzania ili waone kuwa amani ni silaha ya maisha yao ya kila siku
kwani ikivurugika msingi mkubwa wa maisha unaharibika na hakuna hata
mmoja atakayefurahi kuona kuwa amani na upendo vinatoweka.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa viongozi mbalimbali
waliohudhuria mazishi hayo wakiwemo pia maofisa wa Jeshi la Polisi,
wanasiasa, wasomi na watendaji wa Serikali.
No comments:
Post a Comment