MAMA SALMA KIKWETE AMKABIDHI MSAADA WA CHEREHANI YA KUDARIZI MJANE WA MBEYA
Taasisi ya Wanawake na
Maendelea (WAMA) imetoa msaada wa cherehani ya kudarizi kwa mjane Fatma
Almasi ambaye ni mkazi wa Ilomba jijini Mbeya.
Makabidhiano ya Cherehani hiyo yalifanyika hivi karibuni Ikulu jijini Mbeya.
Akimkabidhi cherehani hiyo
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa moja ya kazi
anazozifanya ni kumuinua mwanamke kiuchumi hivyo basi alitoa cherehani
hiyo ili iweze kumsaidia mjane huyo katika maisha yake.
Mama Kikwete alisema kuwa
cherehani hiyo ni moja ya vyerehani walivyovipata kutoka nchini China
kwani watu wanapoomba kusaidiwa siyo kama vitu wanavyovihitaji vipo
bali nao wanatafuta sehemu mbalimbali wakipata wanafikisha kwa
wahitaji.
“Nakutakia kila la heri
katika kazi zako ila usisahau kuleta mrejesho kama kazi inaendelea au
la, isije ikatokea baada ya muda cherehani ikauzwa hiyo siyo maana
yake bali ifanye kazi ya kuzalisha ili nawe uweze kujiinua kiuchumi”,
alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Fatma Almasi
alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada aliompatia kwani amekuwa akihitaji
kuwa na cherehani ya kudarizi kwa kuwa uwezo wa kudarizi anao lakini
hakuwa na kitendea kazi na aliahidi kuongeza cherehani kingine kutokana
na nguvu zake mwenyewe.
Fatma alisema, “Kinamama
tujitahidi kujikwamua kimaisha kwani mwanamke akiwezeshwa anaweza,
tusiwe wategemezi kwa kina baba na mtu asijione kuwa yeye ni mjane au
anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hawezi kufanya jambo lolote na kuona
kuwa ni mwisho wa maisha bali ajitahidi kuwa mjasiriamali kwa kufanya
hivyo ataweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha”.
Aliwaomba wanawake kumuunga
mkono na kumtia nguvu Mama Kikwete kwani ana moyo wa huruma na upendo
wa kuwasaidia kina mama na watoto wa kike.
Taasisi ya WAMA imekuwa
ikiwainua wanawake kiuchumi, kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike
ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha afya ya mama wajawazito
na watoto na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira
hatarishi.
No comments:
Post a Comment