Sunday, June 23, 2013

RAIS WA TFF LEODGER TENGA KUFUNGA KOZI YA MAKOCHA JUMANNE

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodger Tenga anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa kozi ya makocha wa ngazi ya pili (Intermediate) itakayofanyika Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuanzia saa tano asubuhi.

Kozi hiyo iliyodumu kwa wiki nne, ilifunguliwa rasmi Juni 3 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Harbours Club, uliopo Kurasini.

Mkurugenzi wa Ufundi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Joseph Kanakamfumu, alisema Rais Tenga ameridhia kufunga kozi hiyo baada kukosekana katika ufunguzi wa kozi hiyo kutokana na majukumu aliyokuwa nayo.

“Kozi yetu ya ngazi ya pili itafungwa Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa tano asubuhi na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodger Tenga ndiye atatufungia kozi yetu na ameridhia kuwa atakuwa nasi,” alisema Kanakamfumu.

Alisema kozi hiyo itakuwa chachu ya kupatikana kwa makocha watakaosaidia maendeleo ya mchezo huo katika Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Kozi hiyo ni ya kwanza kuendeshwa na DRFA tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya wa chama hicho Desemba 12, chini ya Mwenyekiti Almas Kassongo.

No comments:

Post a Comment