Elikana, Eliud: Watoto walioungana wanaotumia njia moja kujisaidia *Kupelekwa India kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha
Dar es Salaam. “Madaktari waliponiambia kuwa watoto wangu wameungana
nilichanganyikiwa, niliona dunia imenigeuka, sikuwahi kuwaza nitakutana
na kitu cha namna hii katika maisha yangu.”
Ni maneno ya binti kutoka kabila la Wandali ambalo asili yake ni Mbeya,
Grace Joel (19), ambaye Februari 20 mwaka huu, alijifungua mapacha wa
kiume ambao wameungana katika sehemu ya kiunoni.
Mwanadada huyo anasema hakuamini macho yake pale madaktari wa Hospitali
ya Uyole iliyopo mkoani humo walipomwambia kuwa watoto wake wameungana
na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kwenye Hospitali Kuu ya Mkoa wa Mbeya.
"Wakati wa ujauzito wangu sikuwahi hata siku moja kuhisi kuwa ningeweza
kuzaa watoto wakiwa kwenye tatizo hili, sikuwahi kuumwa zaidi ya kuvimba
miguu tu na hiyo ni hali ya kawaida kwa mjamzito yeyote."
anasema
Grace ambaye kwa sasa anahitaji msaada wa hali na mali ili kuokoa maisha
ya watoto wake.
Licha ya umri huo mdogo, amejikuta kwenye hali ya mateso na uchungu
mwingi baada ya familia yake, hususani mume wake, Erick Mwakyusa
kumtelekeza kwa kile alichodai kuwa hana haja na watoto walioungana.
"Nilishangaa, familia yangu kunitelekeza katika hali hii baada ya
kugundua watoto wameungana, mume na familia yake alinitamkia wazi kuwa
hawana shida na watoto walioungana, alisema hawezi kuwalea kwa kuwa kwao
hakuna watoto wenye ulemavu wa aina hiyo,” anasema.
"Siyo siri nilisijikia uchungu, sikuamini kuwa mume wangu angenifanyia
hivyo, siyo yeye tu hata familia yao yote sikudhani kama wangenigeuka
hivyo, nashukuru kwa upande wa familia ya wazazi wangu walikuwa pamoja
nami ingawa ni maskini na hawana uwezo wa kunisaidia.
"Hospitali ya Kyela ndiyo iliyonipeleka ile ya Rufaa Mbeya ambao nao
walivyoona hali ya watoto wangu wakanishauri kuja Muhimbili, sikuwa na
uwezo wa kufika hapa, lakini nawashukuru madaktari wa Rufaa Mbeya
walioniwezesha kufika hapa.
Grace anasema watoto wake hao, Elikana na Eliud aliwazaa wakiwa na uzito
kilo tano na nusu na walifika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki mbili
tangu kuzaliwa kwao.
Wanatumia njia moja kujisaidia
Dk Zaituni Bokhari, ambaye ni Daktari Bingwa katika Kitengo cha Upasuaji
kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, anasema kutokana na namna
walivyoungana, wanatumia njia moja kujisaidia.
"Njia ya kukojolea wanatumia moja na pia njia ya haja kubwa wanatumia
moja, tutakapowatenganisha kuna utaalam ambao utafanywa ili kila mtu
aweze kutumia njia yake mwenyewe bila athari zozote," anasema.
Anaeleza kwamba, iwapo upasuaji huo utafanikiwa watoto hao watakuwa kule
India kwa wiki mbili ndipo watarejea nchini na kuendelea na matibabu
chini ya uangalizi wa wataalamu wa Hospitali ya Muhimbili hadi pale afya
zao zitakapoimarika.
Kutokana na hali ya kiuchumi ya mama huyo, Dk. Bokhari amewataka
wasamaria wema kujitokeza na kutoa misaada mbalimbali kama ya maziwa,
nguo na fedha kwa ajili ya vitu vidogo vidogo ili aweze kuwahudumia
vyema watoto wake.
Dk. Bokhari anasema wao waliwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya
kutokana na uchovu wa safari kwa basi kutoka Mbeya na walikuwa na
maambuzi sehemu mbalimbali.
“Walikuwa ni wachanga kabisa, walikuwa na wiki mbili, walikuwa wamechoka
kutokana na mwendo mrefu wa basi kutoka Mbeya, walikuwa na homa kali na
matatizo katika njia ya kupumua, tukatibu kwanza matatizo hayo ndiyo
vipimo vingine vikaendelea,” anasema.
"Wamefika hapa hawakuwa hata na nguo za kutosha, huyu mama naye alikuja
katika hali ya kuchanganyikiwa ukizingatia ukweli kuwa ndugu zake
wamemtelekeza, tumefanya kazi kubwa sana ya kumpa ushauri nasaha mpaka
akakubalina na hali halisi.
"Kuna wakati alikuwa anasema anataka kuondoka awaache watoto kwetu, hali
hiyo ilitokana na kuchanganyikiwa, muda mwingi alikuwa akilia ila kwa
sasa namshukuru Mungu yeye na watoto wanaendelea vizuri,” anasema.
Kwa nini wameungana
Dk Bokhari anasema hali ya watoto kuungana siyo ya kurithi kama yalivyo kwa baadhi ya magonjwa.
"Hali hii inaweza kusababishwa na upungufu wa madini,” anaeleza.
Mtaalamu mwingine wa afya ameiambia Mwananchi kuwa, “Mapacha wanaofanana
kwa kawaida hutokana na yai lililopandikizwa kujigawa mara mbili, baada
ya siku 12 mgawanyiko wa seli (chembe chembe) unakuwa umeanza kujipanga
kwa ajili ya kujiachanisha katika uumbwaji wa viungo au ogani mbali
mbali za mwili”.
Anasema kuwa, jinsi siku zinavyozidi kusogea mgawanyiko wa mapacha
kujiachanisha na kujitegemea ikitokea kabla ya seli kufikia wakati wa
kuruhusu jambo hilo, ngozi nyembamba za mapacha hao huendelea kuungana
na kushikamana.
“Hata hivyo kwa sayansi ya tiba chanzo kikuu hasa hakijulikani,” anaeleza mtaalam huyo.
Matibabu ni India pekee?
Dk Bokhari anasema kutokana na aina ya upasuaji wa watoto hao, inabidi
ufanyike kwenye nchi zenye watalaamu na vifaa vya kisasa kama India au
Afrika Kusini.
"Upasuaji huu unatakiwa ufanywe na madaktari zaidi ya saba na kila
daktari atakabiliana na kiungo chake, mimi pia ni miongoni mwa madaktari
ambao nitashiriki upasuaji wa watoto hawa na inatakiwa umakini wa hali
ya juu,” anasema.
Anaeleza kuwa, upasuaji wa aina hiyo unaweza kufanyika kwa saa 24 ama chini ya hapo.
SOURCE: MWANANACHI
No comments:
Post a Comment