Friday, June 21, 2013

CRDB YAMPA SHAVU MATALUMA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akipokea mic kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Mataluma baada ya kumtaka aanza kuimba kabla ya msanii huyo kuanza kutoa burudani wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya Wakala wa benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akiimba kibao cha Mataluma kinachokwenda kwa jila la ‘Tunasonga Mbele’. 
 Mataluma akiimba kwa hisia wimbo wa CRDB 'Tunasonga Mbele'
 Wacheza shoo wakionesha manjonjo yao.

DAR ES SALAAM, Tanzania
MSANII wa Bongo fleva kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Mataluma na wacheza shoo wa kundi hilo, walishindwa kuamini baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei kueleza nia ya kununua kibao cha ‘Tunasonga Mbele’.

Kibao hicho kilichotungwa na Mataluma kwa ajili kupamba uzinduzi wa mfumo mpya wa kuhudumia wateja wa CRDB wa FahariHuduma, kilimvutia mno Dk. Kimei na kuagiza idara husika kukaa na msanii huyo kufanya mazungumzo ya kukinunua.

“Nimevutiwa mno na ubunifu uliofanywa na mtunzi katika kibao hiki na ningependa kuona CRDB inakimiliki na kukitumia katika matangazo yetu tofauti, hivyo naiagiza idara husika kukaa na Mataluma na kumlipa, ili asije kukitumia mahali pengine,” alisema Dk. Kimei.
Uamuzi huo ulipokelewa kwa shangwe kutoka kwa waalikwa wa uzinduzi huo, uliofanyika hoteli ya Kempinski, huku wacheza shoo wa THT na Mataluma wakipagawa kutokana na agizo hilo ambalo hawakulitegemea.

Akizungumza baada ya agizo hilo la Dk. Kimei, Mataluma alikiri kufurahishwa kuona utunzi huo umewavutia wengi ukumbini kiasi cha mkurugenzi huyo kukihitaji moja kwa moja, na kwamba anaamini mazungumzo baina ya pande mbili yatafikia muafaka.

 “Nina kila sababu ya kufurahi, kutokana na siku hii kuwa ya aina yake kwangu kama msanii. Namshukuru Dk. Kimei kwa kuvutiwa na kuthamini kilichofanywa katika kibao hiki maalumu kwa ajili ya hafla hii ya uzinduzi wa FahariHuduma ya CRDB,” alisema Mataluma.

Katika uzinduzi huo, Mataluma alikonga vilivyo nyoyo za waalikwa kwa kuimba mashairi yanayoelezea ubora wa huduma za benki ya CRDB, huku wacheza shoo wakionesha umahiri mkubwa wa kumiliki jukwaa. 

No comments:

Post a Comment