Dk Ulimboka ana siri nzito, kuanika kila kitu baadaye, ataka kwa sasa apumzike.
Dk Steven Ulimboka akiwa chumba cha wagonjwa mahututi MOI.
ASEMA ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU
WA JOPO LA MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING’OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA
KUPATA MTIKISIKO WA UBONGO
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara
na kuumizwa vibaya usiku wa kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande,
Dk Steven Ulimboka amesema atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye
na kuomba sasa aachwe auguze maumivu makali yanayomkabili.
Dk Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa
Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na
watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders,
Kinondoni.
Jana, Dk Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku
hali yake ikiwa haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana
maumivu makali anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.
Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
Hata hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji
walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado
limetanda.
Siri nzito
Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka
alisema, akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki
yake ambaye alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika
kwenye klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku
nyingine na kuongeza; “Yaani sikuwa na amani.”
Alisema, “Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu.
Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki,
wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk
Ulimboka),” alieleza na kuongeza:
“Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami,
wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba.”
Hata hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii,
badala yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali
kuhusu hali yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.
Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
“Kidogo najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado
nina maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na
mtu yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi
sasa ni vizuri nipumzike,” ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.
Lakini, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk
Ulimboka, kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona
kiholela siyo tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia
kutowaamini watu ovyo.
Madaktari wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu
tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani,
na hilo tutahakikisha sisi wenyewe,” alisikika akisema mmoja wa
madaktari hao.
Kiongozi jopo la madaktari
Katika hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia
Dk Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa
Dk Ulimboka ana majeraha mwili mzima.
“Ingawa kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana, kwani
mwili wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”
alisema Profesa Kahamba na kuongeza:
“Aliumia mbavuni, kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa
baadhi ya kucha za vidole na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa
meno mawili,” alisema.
Alifafanua kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka
alipata tatizo la mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari
bingwa wanaendelea na harakati za kuokoa maisha yake.
Uongozi wa Moi watoa neno
Uongozi wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea
vizuri ingawa bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha
taasisi hiyo.
Msemaji wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha
ya hali yake kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa
habari kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk. Ulimboka.
“Mgonjwa anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea,
anawatambua watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona
kwa ninyi imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye
utaratibu wake,” alisema Jumaa.
Jumaa aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa
vazi maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu
wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.
Tamko la Jumuiya ya Madaktari
Wakati hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya
uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai
mazingira ya tukio hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa
habari kuwa wangependa kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya
kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma.
“Madaktari kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara, kupigwa
na kutupwa katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume
iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi
kuhusika ama kutohusika kwa jeshi hilo,” alisema Dk Chitage.
Chitage alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku
akionya Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo
hivyo haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.
“Kumekuwa na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini,
hususan Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara
moja na itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine
yoyote bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,” alisema
Chitega na kuongeza:
“Sisi madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania
wakipoteza maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika
mazingira magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya
kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”
Mgomo huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita.