WALIMU WATOBOA MAHUSIANO YA MWENZAO, RPC BARLOW
Baadhi
ya walimu wa Shule ya Msingi Nyamagana wamevunja ukimya na kueleza kile
kinachodaiwa ni mahusiano kati ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Mwanza, Leberatus Barlow, na mwalimu mwenzao, Doroth Moses.
Wakizungumza
na NIPASHE shuleni hapo jana, pia walielezea kusikitishwa kwao na jinsi
tukio hilo la mauaji ya RPC lilivyotokea mbele ya mwalimu mwenzao,
Doroth Moses aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi eneo
la Kitangiri, jijini Mwanza.
Mwalimu
Doroth ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi
Kamanda huyo.
Katika
mahojiano hayo Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mary Ngalula,
alisema wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio
hilo la kutisha.
Alisema
wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa kudhani
anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.
“Tunamuonea
huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia, lakini sisi
tuko pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi, na hivi tunajiandaa
kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake kwani ni
mjane,” alisema.
Mwalimu
Baraka Magafu alisema tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu
uhusiano wa Mwalimu Doroth na Kamanda Barlow, wao (walimu) wanafahamu
kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja huko Vunjo mkoani
Kilimanjaro.
Alibainisha
kuwa Mwalimu Doroth amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na shughuli
mbalimbali za watu wa kabila lake (Wachaga), hivyo hakuna sababu ya
kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu aliyekuwa amemsindikiza nyumbani
wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya harusi aliuawa kwa kupigwa
risasi.
“Ukifuatilia
mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na
kingeweza kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa akimsindikiza Mwalimu
Doroth nyumbani kwake, na hata baada ya tukio, alipowapigia simu wenzao
waliokuwa nao kwenye kikao walikuwa ndipo na wao wanafika majumbani
mwao,” alisema.
Aliongeza
kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa kuwa na mtazamo hasi dhidi
ya Mwalimu Doroth kama ambavyo baadhi ya watu wameanza kuvumisha kuwa
walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Wakati
huo huo, majonzi, simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni mwa
mambo yaliyogubika shughuli ya kuuaga mwili wa Barlow.
Mwili
wa Barlow uliagwa na wakazi wa Jiji la Mwanza wakiongozwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
katika shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana jana.
Baada
ya shughuli ya kuagwa mwili wa Barlow, ulisafirishwa baadaye jana jioni
kwa ndege kuelekea jijini Dar es Salaam kabla ya leo kusafirishwa
kwenda kijijini kwake Vunjo, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
No comments:
Post a Comment