SIR NATURE KUPAGAWISHA ROCK CITY MARATHON 2012
Msanii maarufu wa Bongo Flava, Juma Kassim ‘Sir Nature’ (katikati),
akiimba mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kibao chake kipya cha ‘Narudi
kijijini’ alichomshirikisha Baby Madaha (kulia). Nature atazindua kibao hicho Oktoba
28, wakati wa mbio za Rock City Marathon 2012 zitakazofanyika kwenye Uwanja wa
CCM Kiruma jijini Mwanza. Kushoto ni Mratibu wa Rock
City Marathon,
Grace Sanga.
“Nitatoa burudani safi kwa mashabiki na wanariadha wenyewe watakaoshiriki Rock City
Marathon 2012 jijini Mwanza. Wakazi wote wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla,
wategemee burudani kali na nawataka wajitokeze kwa wingi kushiriki Rock City Marathon”
NYOTA muziki wa Bongo Flava, Juma Kassim ‘Sir Nature,’ leo
ametamba kufanya shoo ya aina yake na kuwapagawisha mashabiki na washiriki wa
mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazofanyika Oktoba 28 kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Sir Nature amesema yeye na kundi lake la Wanaume Halisi wamejipanga
kikamilifu, kuhakikisha wanakata kiu ya kila shabiki na mshiriki wa mbio hizo
zilizo chini ya Uratibu wa Capital Plus International.
“Nitatoa burudani safi
kwa mashabiki na wanariadha wenyewe watakaoshiriki Rock City Marathon 2012
jijini Mwanza. Wakazi wote wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, wategemee
burudani kali na nawataka wajitokeze kwa wingi kushiriki Rock City Marathon.
“Kwa kuwa michezo ni afya, nategemea wakazi wengi wa Mwanza
na vitongoji vyake watatumia muda uliobaki kujisajili ili wawe sehemu ya tukio hilo muhimu maishani
litakalofanyika Oktoba 28, ndani ya dimba la CCM Kirumba,” aliongeza Sir Nature.
Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo Grace Sanga wa Kampuni
ya Capital Plus International (CPI), alisema kuwa maandalizi yanaendela vizuri
huku akisema mbio za mwaka huu zimeboreshwa zaidi ukilinganisha na za mwaka
jana.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na natumia nafasi hii kuomba
wananchi ambao mpaka sasa hawajajitokeza kusajiliwa, kufanya hivyo haraka kuwahi
muda na nafasi zilizosalia. Natumia nafasi hii pia kutoa shukrani kwa wadhamini
wetu kwa kutuunga mkono,” alisema Grace.
Rock City Marathon 2012 ni mbio hizo zilizo chini ya
udhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Airtel Tanzania, Bodi
ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottles, PPF, Geita Gold
Mine, TANAPA, Sahara Communication, ATCL, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.
Aidha, Grace aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuchukua fomu
za usajili kwenye Ofisi za Uwanja wa Nyamagana Mwanza, Ofisi za Capital Plus
International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, Ofisi za Bodi ya
Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar
es Salaam, pia kupitia tovuti ya
www.rockcitymarathon.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment