Mke wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda Mama Tunu Pinda naye ahitimu Shahada ya Uongozi wa Biashara
Mkuu
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, John Samwel Malecela akimtunuku
Shahada ya Uongozi wa Biashara, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda
katika Mahafali ya Chuo Kikuu Huria yaliyofanyika kwenye viwanja vya
Chuo hicho Kibaha Oktoba 27, 2012.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
----
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wahakikishe kuwa wao wenyewe na
watoto wao wanatumia fursa ya kudahiliwa kwenye Chuo Kikuu Huria badala
ya kuendelea kusubiri mabweni yajengwe kwenye Vyuo Vikuu.
“Kama
tutasubiri mashirika na taasisi za dini au watu binafsi wajenge vyuo
vikuu vya mabweni, ni dhahiri wanafunzi wengi wasio na uwezo wa kulipia
ada katika vyuo hivyo watasubiri kwa muda mrefu ili wadahiliwe au wakose
kabisa nafasi kwenye Vyuo Vikuu,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 27, 2012) wakati
akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT) yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho eneo la
Bungo, wilayani Kibaha, Pwani.
Alisema
kuwepo kwa Chuo Kikuu Huria kumetoa fursa ya kuongeza udahili wa
wanafunzi kwenye vyuo vikuu kwa kiwango kikubwa kwa vile kinaweza
kuchukua wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.
“Napenda
kuwasihi wananchi kujiunga na chuo hiki kutokana na ubora wa elimu
inayotolewa pamoja na uhakika wa kuendelea na shughuli za kazi, ajira
binafsi na kumwezesha mtu kukaa pamoja na familia,” alisema.
Waziri
Mkuu aliahidi kufuatilia ombi la ujenzi wa barabara ya lami iendayo
kwenye chuo hicho ambayo haizidi kilometa nne ili ikamilike mapema. Pia
alimtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
ashirikiane na Wakala wa Majengo (TBA) kuharakisha upatikanaji haraka wa
majengo mikoani kwa taratibu zinazokubalika ili yasaidie kutatua tatizo
la vituo vya kufundishia wataalamu mikoani.
Jumla
ya wahitimu 2,787 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada za kwanza, na
stashahada za juu katika fani za Sayansi ya Jamii, Ualimu, Elimu
Maalum, Biashara na Fedha, Sayansi, Sheria, Uhasibu, Uchumi, Mazingira,
Utalii, Masoko, Kiswahili, Utawala, Uandishi wa Habari na Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano.
Miongoni
mwa viongozi waliohitimu jana ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda
aliyehitimu Shahada ya Uongozi wa Biashara na Biashara ya Kimataifa (BBA
– International Business). Wengine ni wakuu wa mikoa ya Shinyanga na
Simiyu, Bw. Ali Nassoro Rufunga na Bw. Pascal Mabiti wakiwemo pia Mkuu
wa Wilaya ya Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla na Mbunge wa
Tandahimba, Bw. Juma Njwayo.
Akihojiwa
na waandishi wa habari mara baada ya kupatiwa shahada yake, Mama Tunu
Pinda alisema anawasihi wanawake wote wajiendeleze bila kujali wako
kwenye nafasi ipi kwani elimu haina mwisho. “Umuhimu wa elimu hauangalii
kama wewe ni mke wa kiongozi au la, elimu inawahusu watu wote!,”
alisema.
Alisema
mahafali hayo yamempa hamasa ya kusoma tena zaidi na zaidi kwani ameona
wahitimu wengine wakipata shahada za juu zaidi. “Nimeona wenzagu
wakipokea Ph.D zao nikasema mimi nina Bachelor tu, hapana. Lazima niende
mbele zaidi,” alisema bila kufafanua kuwa atasomea fani gani.
Mapema,
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Prof. Samwel Wangwe alisema Chuo
hicho tayari kinashirikiana na vyuo vingine vya elimu ya juu vya umma
hapa nchini kama SUA, MUHAS, DIT na CBE ili kuongeza udahili wa
wanafunzi vyuoni.
Alisema
chuo hicho kina mpango wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano
kwa kuchapisha vitabu vya kujisomea kwenye CD na DVD ili kupunguza
gharama za uchapishaji wa vitabu.
Aliziomba
wizara zenye majengo yasiyotumika huko mikoani ziyatoe kwa chuo hicho
ili yafanyiwe ukarabati na yaweze kutumika kutoa elimu kwa wataalam
wengi zaidi nchini.
Alitumia
fursa hiyo kuiomba Wizara ya Ujenzi waiingize barabara iendayo stesheni
ya Soga kupitia chuoni hapo katika mpango wake wa muda mfupi ili
iwekewe lami na hivyo kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Tolly Mbwete alisema Chuo hicho kina
eneo la ekari 105 na kwamba kinatarajia kuanza ujenzi wa majengo mawili
kwa ajili ya madarasa na ofisi za chuo ambao utagharimu sh. bilioni
15/-.
Kuhusu
changamoto zinazokikabili Chuo hicho, Prof. Mbwete alisema wanakabiliwa
na changamoto ya uhaba wa rasilmali fedha, uhaba wa mabweni na uhaba wa
wanataaluma. Aliomba wapatiwe fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu
yake. Aliomba kuwe na ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili wapatiwe fedha za malimbikizo ya
mishahara ya wafanyakazi wa chuo hicho.
No comments:
Post a Comment