TENGA AKATAA KUJIUZULU KWA RANGE
Kumekuwepo
na taarifa tofauti kuhusu kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara ambayo kwa
mujibu wa kalenda ya Shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), inatakiwa kuanza Septemba 01, 2012. Baada ya kikao cha pamoja
baina ya TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika Jumatatu
ya Agosti 20, 2012 kwenye ofisi za TFF, TFF inapenda kutoa ufafanuzi
ufuatao:
1. Baada
ya kikao cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu
zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa
mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa, yaani
Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii
inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande
husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2. Mazungumzo
baina ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo
mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa
mazungumzo hayo.
3. Kukamilika
kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila
ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa
kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika
kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa
muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na masuala mengine
muhimu.
4. Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu
5. Kutokana
na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao
ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao
sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa
Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku
itakayotangazwa baadaye.
6. Kuhusu
chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya
Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu
kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya
TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili
ya hatua za mwisho.
SEMINA KWA AJILI YA MAKAMISHNA, WAAMUZI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina kwa ajili ya
makamishna (match commissioners), watathmini wa waamuzi (referees
assessors) na waamuzi wa daraja la kwanza (class one) ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao.
Kwa
upande wa makamishna na watathmini wa waamuzi, semina itafanyika
jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 29-30 mwaka huu. Washiriki
wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri, malazi na chakula
wawapo kwenye semina.
Semina
kwa waamuzi itafanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza
kuanzia Agosti 31- Septemba 2 mwaka huu. Pia nao watajigharamia kwa
kila tu. Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni ambao hawakushiriki ile
iliyofanyika Juni mwaka huu na wale walioshiriki lakini hawakufaulu
mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test).
Waamuzi
wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
hawashiriki kwa vile wao wamekukuwa wakishiriki semina zao
zinazoandaliwa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.
TENGA AKATAA KUJIUZULU KWA RAGE
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa
barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.
Rage
ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga
barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo
kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira
Tanzania zinavyoeleza.’
Amekataa
ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa
kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea
kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia kusimamia sheria na kanuni hizo
kama inavyotakiwa badala ya kujiuzulu.
“Kutokana
na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu,
ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama
inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu
za maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga.
Pia
Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa
kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati zote
za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala
kupendelea upande wowote.
Rais
Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili
bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati
zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo,
uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa
miguu kuongozwa kwa sheria na haki.
No comments:
Post a Comment