Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison
Mwakyembe amesema huduma za treni Dar es salaam kwa kuanzia zitakua
kutoka stesheni ya reli Dar es salaam hadi Ubungo maziwa ikiwa ni
kilomita 12 pamoja na Mwakanga hadi Kurasini kupitia stesheni ya Dar es
salaam kilomita 34.5.
Amesema “kazi ya ukarabati wa
njia na injini tatu za treni na mabehewa 14 ya abiria imeanza na
inatarajiwa kukamilika oktoba 2012 ambapo huduma hii itaanza kwa kuwa na
treni mbili ambazo zitatoa huduma asubuhi na jioni kuanzia jumatatu
mpaka jumamosi”
Dr Mwakyembe ambae amepata
pongezi kubwa pia baada ya kufichua uozo kwenye shirika la ndege
Tanzania, amesema Treni hizo zitasimama kwenye vituo sita ambavyo ni
stesheni ya Dar es salaam, Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata
Matumbi, Mabibo na Ubungo Maziwa na kila treni itakua na mabehewa sita
yenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa na waliosimama elfu moja kila
safari na inakisiwa treni hizo zitaweza kusafirisha watu elfu kumi na
sita kwa siku.
Baada ya kusema hayo, Dr
Mwakyembe amewasihi wafanyabiashara kuwekeza kwenye mradi wa maegesho ya
magari kwenye eneo la eka nne Ubungo lililotengwa kwa ajili ya watu
wanaotoka Kibaha, Kimara, Kiluvya, Mbezi Luis na kwengine kwa ajili ya
kupaki magari yao Ubungo kisha kupanda treni kwenda stesheni ya Dar es
salaam.
Kwa upande wa reli ya Tazara
ukarabati wa injini tatu na treni za mabehewa 14 unaendelea na
unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu ambapo huduma hiyo ya treni
itakua na njia mbili, Mwakanga kwenda Yombo mpaka stesheni ya Tazara
ikichukua dakika 30 alafu njia ya pili Mwakanga kwenda Yombo mpaka
Kurasini ikichukua dakika 40, itakua na vituo 14 ambavyo ni stesheni ya
Tazara, kwa fundi umeme, Yombo, Kwa Limboa, Lumo, Kigilagila, Barabara
ya Kitunda Kipunguni B, Moshi Bar, Majohe, Shule ya sekondari Magnus,
Mwakanga, Chimwaga, Maputo, Mtoni relini, Kwa Aziz Ally relini hadi
Kurasini.
Akisoma bajeti mpya ya wizara
ya Uchukuzi, Dr Mwakyembe amesema ili kuimarisha na kuboresha utendaji
wa TRL Wizara imetenga shilingi bilioni 104 kwenye bajeti ya 2012/2013
zitakazotumika kwenye miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzijenga
upya injini 8 za treni, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa treni mpya
13, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa Mabehewa mapya ya abiria 22,
kukarabati mabehewa mabovu ya mizigo 125, kufanya malipo ya awali ya
ununuzi wa mabehewa mapya ya mizigo 274, kufanya malipo ya awali ya
ununuzi wa mabehewa mapya ya breki
34 na ukarabati wa karakana za Tabora na Dar es salaam ambapo katika
fedha hizo shilingi bilioni 18.9 zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni
ya kimkataba na IFC ya Uganda na wadai wa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment