Monday, April 1, 2013

*TASWA FC, TASWA QUEENS ZANG'ARA BONANZA LA PASAKA DAR


Mwandishi wetu
TIMU ya soka na Netiboli za Waandishi wa Habari za michezo nchini, Taswa FC na Taswa Queens zimemaliza maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka kwa kishindo baada ya kuwatambia wageni wao, timu ya Kiliflora ya Arusha.
Katika mchezo wa soka, uliochezwa kwenye uwanja wa TCC Chan'ombe Taswa FC iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 wakati katika mchezo wa netiboli uliochezwa pia kwenye uwanja huo huo, Taswa Queens iliyokuwa inacheza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 iliibuka na ushindi wa mabao 28-8.
Taswa FC ilianza mechi hiyo kwa kasi na kufana mashambulizi ya mengi hata hivyo, washambuliaji wake, Julius Kihampa na Shafii Dauda walikosa mabao mengi ya wazi.
Katika mechi hiyo, kipa wa Taswa FC, Said Seif alikuwa ‘likizo’ kufuatia safu ya ulinzi chini ya Muhidin Sufiani, Fred Mweta, Sweetbert Lukonge, Fred “Chuji” Mbembela kuwa imara muda wote huku safu ya kiungo ilichezwa na Ali Mkongwe, Wilbert Molandi, Majuto Omary na Evarist Hagila kutotoa mwanya kwa Kiliflora kupenya na kupeleka mashambulizi.
Baada ya kosa kosa hizo, Taswa FC iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 24 kufuatia gonga safi za Majuto “Ronaldo De Lima” Omary na Ali Mkongwe kabla ya mpira kumfikia Hagila na kuuweka kimiani.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya Kiliflora na kujikuta wakipachikwa bao la pili kupitia kwa Dauda baada ya pasi nzuri ya Wilbert Molandi  aliyecheza vyema na Sweetbert Lukonge na kufanya timu hiyo kuongoza kwa mabao 2-0 mpaka mapumziko.
Taswa Fc ilifunga bao la tatu kupitia kwa Hagila baada ya pasi kupata pasi safi ya Fred Mbembela ‘Chuji’ na baadaye Dauda kufunga la bao la nne kufuatia ngazi nzuri ya Majuto.
Katika netiboli, ikiongozwa na Imani Makongoro aliyecheza nafasi ya (GS), Taswa Queens iliifunika kabisa Kiliflora Queens baada ya kuongoza kwa 16-3 hadi Mapumziko.
Wachezaji wengine wa Taswa Queens waliocheza mechi hiyo mbali ya Imani ni Oliver (mwananchi), Sada Ayoub,  Johari William, Elizabeth Mbassa, Shaarifa Mustapha wote wakitokea Business Times. Timu hiyo ilikuwa chini ya makocha, Amina Mussa (BTL) na Zainab Ramadhan (TBC).
 Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto akikagua timu ya Netiboli ya Kiliflora ya Arusha, kabla ya kuanza kwa mchezo huo jana.
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, akikagua timu ya Netiboli ya TASWA Queens, kabla ya kuanza kwa mchezo huo jana.
Picha ya juu ni TASWA Fc katika picha ya pamoja na ya chini ya 
Kiliflora ya Arusha, kabla ya kuanza kwa mchezo huo jana.

*TIMU YA BARRACK YOUNG CONTROLLER II KUWASILI KESHO KWA MARUDIANO NA AZAM APRIL 6 DAR


Kikosi cha Azam Fc.

Timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia inatarajia kuwasili nchini kesho (Aprili 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam itakayochezwa Jumamosi (Aprili 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Young Controllers itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.
Msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 37 wakiwemo wachezaji 21 na utaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo Robert Alvin Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.
Wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy, Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.
Benchi la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu Robert Lartey akisaidiwa na Samuel Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel Massaquoi.
Timu hiyo inatarajia kuondoka kurejea Monrovia, Aprili 8 mwaka huu kupitia Nairobi, Kenya saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir.

No comments:

Post a Comment