MATOKEO YA DARASA LA SABA UFAULU NI ZAIDI YA MWAKA JANA
Takwimu
za matokeo hayo zikionyesha kuwa zaidi ya nusu wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 ni wale waliopata asilimia 40
ya alama kwenda chini katika matokeo hayo.
Katika
matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wananfunzi 294,833 sawa na asilimia asilimia
52.58 waliopata daraja ‘D’ wamechaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza.
Hao wanaungana na wenzao 265,873 waliopata madaraja ya A,B na C ambao
ni sawa na asilimia 47.41. Kwa mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa
la saba, jumla ya alama zote ni 250 ambazo zimegawanywa katika madaraja
matano ambayo ni A mpaka E.
Mchanganuo wa madaraja hayo ni alama 201 hadi 250 kwa daraja la A,
alama 151 – 200 kwa daraja B, alama 101 hadi 150 kwa daraja C, alama 51 –
100 kwa daraja D na alama 0 – 50 kwa daraja E.
Waziri Kawambwa alisema wanafunzi 560,706 walichaguliwa kuendelea na
elimu ya sekondari kati ya 865,534 waliofanya mtihani huo wa siku mbili;
Septemba 19 na 20 mwaka huu na kwamba mwaka huu wasichana wamefanya
vizuri katika mtihani huo kuliko wavulana.
“Wasichana waliofaulu ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 ya wanafunzi
560,706 wakati wavulana waliofaulu ni 279,246 sawa na asilimia 49.80,”
alisema Kawambwa alipokuwa akitangaza matokeo hayo na kuongeza:
“Matokeo yanaonyesha kuwa jumla ya wahitimu 3,087 walipata daraja A,
wakati 40,683 walipata daraja la B. Wanafunzi 222,103 walipata alama za
daraja C wakati 526,397 walipata daraja D. Watahiniwa waliobaki 73,264
walipata E”.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga
na kidato cha kwanza mwaka 2013, imeongezeka kwa asilimia 8.8
ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa mwaka jana.
“Mtihani wa mwaka huu, kwa mara ya kwanza watahiniwa walifanya kwa
kutumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) na ulisahihishwa
kwa kutumia kompyuta,” alisema.
Alisema matokeo haya yanaonyesha alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
Kabla ya matokeo, wasichana waliofanya mtihani walikuwa 456,082 sawa
na asilimia 52.68 na wavulana ni 409,745 sawa na asilimia 47.32,”
alisema Dk Kawambwa.
“Watahiniwa 29,012 sawa na asiliamia 3.24 hawakufanya mtihani
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo na ugonjwa,” alisema.
Dk Kawambwa alisema, kati yao, ambao hawakufanya mtihani wasichana
walikuwa 12,501 sawa na asilimia 2.67 na wavulana ni 16,511 sawa na
asilimia 3.87.
Waziri huyo alisema, udanganyifu katika mitihani kwa mwaka huu
umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana.
“Waliofutiwa matokeo mwaka huu ni watahiniwa 293 ikilinganishwa na
watahiniwa 9,736 waliofutiwa matokeo yao kwa udanganyifu mwaka jana,”
alisema Dk Kawambwa.
Katika
Mtihani huo Jumla ya wanafunzi 894,881 walisajiliwa kufanya mtihani huo
ambapo wavulana ni 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni
468,596 sawa na asilimia 52.36.
Aidha,
kati ya wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379 ambao walitarajiwa
kufanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502
walitarajiwa kufanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia
kujifunzia.
Wanafunzi
wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na
wasichana 39. Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi
makubwa ni 495, kati yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.
No comments:
Post a Comment