Saturday, December 22, 2012

.
Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es salaam jana december 21 2012 imefunga jalada la kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili mwigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu tayari kwa kulipeleka Mahakama kuu ya Tanzania ili hiyo kesi ianze kusikilizwa.

Kabla ya kusomwa kwa maelezo ya kesi hiyo ambapo Lulu hakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Kisutu Augustina Mmbando amemtaka wakili wa serikali kutaja idadi ya mashahidi watakaotoa ushahidi wao wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.

Wakisoma kwa awamu maelezo ya mashahidi wa kesi hiyo, mawakili wa serikali kwenye hiyo kesi wamesema wanao mashahidi tisa wanaotarajiwa kuwatumia kwenye kesi na kuongeza kwamba shahidi namba moja ni Seth Bosco mdogo wa Marehemu Kanumba waliekua wakiishi pamoja.

Kwenye maelezo yaliyosomwa na Seth mahakamani, imeelezwa kwamba siku ya tukio Kanumba alimtaka asitoke ili watoke pamoja baadae lakini ilipofika saa tano usiku alisikia vurugu chumbani kwa Kanumba ambako alikua na mpenzi wake ambae ni Lulu na baada ya muda Seth aligundua kulikua na ugomvi unaendelea na mlango ulikua umefungwa.

Maelezo hayo yameendelea kwamba baada ya muda Lulu alitoka chumbani kwa Kanumba na kumtaarifu Seth kwamba Kanumba ameanguka ambapo Seth alipoingia chumbani alikuta Kanumba kaegemea ukuta pembezoni mwa mlango huku povu likimtoka mdomoni na kuamua kumlaza chini kabla ya kuomba msaada.

Mashahidi wengine wanaotarajiwa kutoa ushahidi wao wakati kesi itakapoanza kusikilizwa ni Sophia Kassim ambae ni mmiliki wa nyumba aliyokua anaishi Kanumba, madaktari watatu, Polisi watatu, afisa uhamiaji ambae ni shemeji wake Kanumba na Moris Sekwao ambae ni kijana aliempakia Lulu kwenye gari lake muda mfupi kabla ya kukamatwa.

Baada ya kusomwa kwa maelezo ya mashahidi wote, wakili wa serikali amesoma maelezo ya Lulu na kuamplfy kwamba mwigizaji huyu alianza uhusiano wa kimapenzi na Kanumba january 2012 ambapo walikua na kutoelewana katika baadhi ya nyakati hasa pale mmoja anapompigia simu mwenzake na haipokelewi kwa wakati.

Baada ya maelezo yote kutolewa na kukamilika, Hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Augustina Mmbando amezishukuru pande zote na kumtaka Lulu atoe maelezo ya nyongeza kama anayo ambapo Lulu alisema hana maelezo yoyote ya kuongezea.

Hakimu Mmbando amemtaka Lulu kuendelea kubaki rumande mpaka tarehe ya kesi yake itakapotajwa na Mahakama kuu ya Tanzania.

Hakuna ukweli wowote wa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Lulu ameachiwa kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment