Polisi wakati wa fujo za Mtwara.
Taarifa ikufikie kwamba Waziri
mkuu Mizengo Pinda amefanikiwa kutuliza jazba za wakazi wa Mkoa wa
Mtwara kwa kuwaeleza kuwa kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa
kijijini Madimba mkoani humo ili mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike
kuvutia uwekezaji wa viwanda, hii ikiwa ni kauli tofauti na ya madai ya
wakazi hao ambao hasira zao zilichangiwa na taarifa kwamba kiwanda
hicho kingejengwa Dar es salaam.
Kwenye mkutano wa majumuisho
uliofanyika january 29 2013 Waziri mkuu baada ya kusikiliza madai ya
wananchi hao kwa siku mbili mfululizo, amesema hakuna tone la gesi ghafi
itakayosafirishwa kwa njia ya bomba.
Namkariri akisema “Imani yangu
ni kwamba maelezo yametosheleza, mtakua na kiwanda chenu cha kusindika,
mtakua na kiwanda cha kusafisha, mtakua na hayo matawi kadhaa kwa ajili
ya uzalishaji wa umeme kwa ajili ya usindikaji wa viwanda”
Mwanzoni madai ya wakazi wa
Mtwara yalikua ni kupinga usafirishaji wa gesi ghafi mpaka Dar es salaam
wakieleza kwamba huo mpango utafukuza wawekezaji wa viwanda Mtwara
ambao ungechochewa na upatikanaji wa malighafi baada ya kusafishwa kwa
gesi.
Jengo la Mahakama lililotelekezwa.
Pia wananchi walipinga ujenzi
wa mitambo ya kuzalisha umeme kinyerezi Dar es salaam na badala yake
wakataka hiyo mitambo ijengwe hukohuko Mtwara.
Kwenye mstari mwingine Waziri
Mkuu aliwataka wananchi kumsamehe mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali mstaafu
Joseph Simbakalia kwa kauli alizotoa december 21 2012 katika kikao cha
kamati ya ushauri pale alipoombwa kuyapokea maandamano ya wakazi wa mkoa
huo december 27 ambapo aliwaita wapuuzi na wahaini.
Waziri mkuu katika majumuisho
yake aliambatana na Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya kazi profesa
Anna Tibaijuka, Waziri wa Uchukuzi Dr. Harrison Mwakyembe, Waziri wa
elimu na mafunzo ya ufundi stadi Dr. Shukuru Kawambwa na Waziri wa mambo
ya ndani Dr. Emmanuel Nchimbi.
Katika hizo siku mbili pia
Waziri mkuu alikutana na vyama vya siasa vya upinzani, chama cha
Mapinduzi CCM, viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo,
Wafanyabiashara, Madiwani na wenyeviti wa mitaa pamoja na Wanaharakati.